1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la usalama kujadili mabadiliko ya hali ya hewa

Josephat Charo11 Aprili 2007

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ambalo kazi yake kubwa ni kuzuia vita na kulinda amani ya dunia, kwa mara nyengine tena litavunja utamaduni wake Jumanne wiki ijayo kujadili mabadiliko ya hali ya hewa ambyo imeelezwa kuwa hatari mpya inayoukabili usalama wa kimataifa.

https://p.dw.com/p/CHlF
Kikao cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani
Kikao cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York MarekaniPicha: AP

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 15, ambalo kwa kawaida hujihusisha sana na siasa za kimataifa, kwa mara kadhaa limejadili maswala mengine kama vile haki za kijinsia, ugonjwa wa ukimwi na juhudi za kulinda amani duniani. Lakini maswala haya matatu yalijadiliwa kwa sababu kwa njia moja au nyengine yanahusiana na hali ya mizoizo au amani ya kimataifa na usalama.

Catherine Pearce, mwanaharakati wa mabadiliko ya hali ya hewa katika shirika la kimataifa la kuyalinda mazingira la Friends of the Earth, amesema shirika lake linaunga mkono mpango uliowasilishwa na serikali ya Uingereza kujadili mabadiliko ya hali ya hewa kwenye mkutano ujao wa baraza la usalama utakaofanyika tarehe 17 mwezi huu.

Christine Pearce ameliambia shirika la habari la IPS kwamba bila shaka wanayachukulia mabadiliko ya hali ya hewa kuwa hatari kubwa ambayo haiyakabili tu mazingira bali pia binadamu, uchumi na usalama. Lakini cha muhimu ni kwamba mazungumzo ya ngazi ya juu kama yale yatakayofanywa na baraza la usalama, yanafuatiwa na vitendo. Ni mataifa yaliyoendelea kiviwanda yanayotakiwa kufanya mengi zaidi kupunguza utoaji wa gesi za viwandani, hususan Marekani, na hatua kali zaidi zinahitajika kuchukuliwa.

Christine Pearce amesema msaada zaidi na fedha nyingi zinahitajika na mataifa maskini yanayokabiliana na athari zilizosababishwa na ongezeko la joto duniani. Katika mkutano na waandishi wa habari wiki iliyopita, mjumbe wa Uingereza, Emyr Jones Parry, ambaye ni rais wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mwezi huu wa Aprili, alisema hatua ya kuwa na mkutano unaozungumzia mabadiliko ya hali ya hewa ni muhimu.

Hata hivyo Parry alisema madai kwamba Uingereza ni kiongozi katika maswala ya mabadiliko ya hali ya hewa yanapotosha. Bila shaka Uingereza inataka kuwa msitari wa mbele lakini kila mtu anatakiwa kufanya hivyo kwa kuwa swala la mabadiliko ya hali ya hewa ni kubwa na haliwezi kuachiwa nchi moja pekee. Parry alisema huenda kukafanyika mkutano wa kilele wa kimataifa utakaozungumzia mabadiliko ya hali ya hewa mwaka ujao.

Atakayekuwa mwenyekiti wa mkutano huo wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ni waziri wa mashauri ya kigeni wa Uingereza, Margaret Beckett. Katika mkutano huo lakini hakuna mpango wowote wa kutoa taarifa za rais au kupitisha azimio juu ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Philip E Clapp, kiongozi wa shirika la mazingira la National Environment Trust, amesema ripoti iliyotolewa Ijumaa iliyopita na jopo la kiserikali linalohusika na mabadiliko ya hali ya hewa, IPCC, itasababisha mijadala mikubwa juu ya viwango vya uthabiti wa kisiasa wa kimataifa na mizozo ya kikanda. Kwa hiyo ni muhimu kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kukabiliana na athari.

Aidha bwana Clapp amesema barani Afrika pekee mamilioni ya watu huenda wakakabiliwa na baa la njaa kutokana na kupungua kwa kiwango cha mazao.