Baraza la Usalama kuijadili Nicaragua
5 Septemba 2018Kikao hicho cha jumatano kimeitishwa kwa pendekezo la Marekani kitajadili juu ya wasiwasi unaoongezaka kutokana na jinsi serikali ya nchi hiyo inavyoshughulia wakosoaji wake ikiwemo waandamanaji wa maandamano dhidi ya serikali yaliyoanza tangu Aprili 18.
Bolivia ambayo ni mshirika muhimu wa Nicaragua na mjumbe asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama imesema itajaribu kuzuia mjadala juu ya Nicaragua lakini balozi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Nikki Halley amesisitiza kuwa ni muhimu kwa ulimwengu na Baraza hilo kufahamu kile kinachoendelea ndani ya nchi hiyo.
Nicaragua imetumbukia kwenye mzozo wa kisiasa tangu maandamano dhidi ya serikali yalipozuka mwezi Aprili ambapo vurugu na ukandamizaji wa serikali umesababisha kiasi vifo 300 na watu wengine zaidi ya 2000 kujerehiwa kulingana na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa katika ripori yake ya wiki iliyopita.
Kadhalika ripoti hiyo imeeleza kuwa zaidi ya watu 1200 wamekamatwa kinyume cha sheria au wamepotea kwenye mazingira ya kutatanisha.
Wakosoaji wa Serikali bado wanalengwa
Msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Liz Throssel amesema katika wiki za hivi karibuni watu na makundi yanayonasibishwa na maandamano dhidi ya serikali wameendelea kukamatwa na vyombo vya habari nchini humo wamewapa jina la kuwa magaidi na wapanga njama ya kupindua serikali.
Wiki iliyopita serikali ya rais Daniel Ortega iliamuru kufukuzwa kwa ujumbe wa Ofisi ya Haki za binadamu siku mbili tangu ilipochapisha ripoti iliyokosoa kile ilichokiita hali ya hatari katika taifa hilo la Amerika ya kati.
Wajumbe wote wanne walioagizwa Nicaragua na ofisi ya kamishna wa haki za binadamu wakiongozwa na Guillermo Fernandez waliondoka muda mfupi baadae kueleka Panama ambapo kuna ofisi ndogo ya chombo hicho.
Katika ripoti yake ujumbe huo umetaja masuala lukuki ya ukatili uliopindukia nchini humo ikiwemo matumizi makubwa ya nguvu kutoka kwa polisi ambayo katika baadhi ya visa yamesababaisha mauaji, kupotea kwa watu, kuwekwa watu kwa nguvu kizuizini na mateso.
Rais Ortega ambaye ni mpiganaji wa zamani wwa vita vya msituni aliyeitawala Nicaragua kwa miaka 11 iliyopita amepuuza madai hayo na kuutaja Umoja wa Mataifa kama chombo cha sera za hatari uongo na uzushi.
Ofisi ya Haki za Binadamu itaendelea kufuatilia
Licha ya kutimuliwa kwa ujumbe wake nchini humo ofisi ya haki za binadamu imesema itaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya haki za binadamu kupitia njia zote zinazowezekana
Kwa mujibu wa msemaji wa ofisi hiyo katika nchi ambazo ujumbe wa wataalam wa chombo hicho umezuiwa kufanya kazi, ofisi hiyo ya haki za binadamu yenye makao yake mjini Geneva huwasiliana na wahanga, wanaharakati na vyanzo vingine kupitia njia tofauti za mawasiliano.
Mwandishi: Rashid Chilumba/DPAE/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman