Baraza la mpito kuiongoza Yemen
20 Februari 2015Makubaliano hayo yanakuja baada ya vuguvugu la kundi la wanamgambo wa Kishia la Wahouthi kunyakuwa madaraka nchini humo na kupelekea kujiuzulu kwa kwa rais wa nchi hiyo hapo mwezi uliopita na kusababisha taasisi nyingi za serikali kushindwa kufanya kazi.
Mpatanishi wa Umoja wa Mataifa kwa mzozo huo wa Yemen, Jamal Benomar, amesema katika taarifa yake kwamba licha ya kuwa hatua hiyo sio makubaliano ya mwisho, lakini ni ufumbuzi muhimu unaofunguwa njia ya kufikia makubaliano kamili.
Kama sehemu ya makubaliano hayo mapya, bunge la Yemen lenye wabunge 301 ambao wengi wao ni wanachama wa chama tawala cha zamani ambacho kinafikiriwa kilikuwa kikiwapendelea Wahouthi litarudishwa madarakani baada ya kuvunjwa.
Maudhui ya makubaliano
Baraza la juu la bunge ambalo ni baraza jipya la mpito ambalo idadi yake haikutajwa litajumuisha makundi ambayo kawaida hayawakilishwi katika baraza hilo kutoka Yemen ya kusini wakiwemo wanawake na vijana.
Kwa pamoja mabaraza hayo mawili ndio yatakayotunga sheria zitakayoingoza Yemen wakati wa kipindi cha mpito.
Kwa mujibu wa Benomar mwanadiplomasia kutoka Morocco masuala ya nyadhifa za urais na wizara pamoja na usalama yanahitaji kujadiliwa zaidi.Hakuna maelezo yoyote yaliopatikana mara moja kutoka kwa kundi la Wahouthi au makundi mawili makuu ya Waislanu wa itikadi kali wa madhehebu ya Sunni kuzungumzia makubaliano hayo.
Usalama unazidi kuzorota
Usalama nchini Yemen umekuwa ukizidi kuzorota tokea Wahouthi walipouvamia mji mkuu wa nchi hiyo Sanaa hapo mwezi wa Septemba na kuanza kuweka amri zao kwa serikali.
Taifa lenye ushawishi mkubwa katika kanda hiyo Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na nchi nyengine kadhaa duniani zimefunga balozi zao mjini Sanaa na zinahofia ombwe la madaraka nchini humo yumkini likawapa nguvu tawi la al-Qaida nchini humo na hata kuchochea vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa misingi ya madhehebu.
Unyakuzi wa madaraka wa Wahouthi umelaaniwa kuwa ni mapinduzi na makundi ya kadhaa ya kisiasa nchini humo na kuzusha maandamano ya umma hususana kutoka Wasunni walio wengi nchini humo.
Kundi la Wahouthi limechipukia kama vuguvugu la kufufuwa mila za Wayazidi wa madhehebu ya Shia ambao kihistoria wamekuwa wakidhibiti nyanda za juu kaskazini mwa Yemen. Hapo mwezi wa Januari walimweka Rais Abdu Rabu Mansour Hadi kwenye kifungo cha nyumbani na kuilazimisha serikali kujiuzulu.
Yemen ni mojawapo ya nchi maskini kabisa katika ulimwengu wa nchi za Kiarabu na ni ngome madhubuti ya tawi la al-Qaida.
Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters/dpa
Mhariri: Mohammed Khelef