Baraza la mawaziri laidhinisha punguzo la euro bilioni 11.2
7 Juni 2010Baraza la mawaziri la Ujerumani limekamilisha leo mipango ya kupunguza matumizi ya serikali ya shirikisho kwa kiasi cha Euro bilioni 11.2 sawa na dola za Kimarekani 13.3 bilioni katika mwaka 2011.
Mikasi mengine zaidi itafuata katika miaka mitatu ijayo na kufikia kiasi cha Euro bilioni 19.1 katika mwaka 2012, Euro bilioni 24.7 katika mwaka 2013, na Euro bilioni 26.6 ifikapo mwaka 2014. Katika kikao maalum cha siku mbili kilichoanza jana cha baraza la mawaziri kilichofanyika katika ofisi ya kansela Angela Merkel , mawaziri pia wameidhinisha kupunguzwa Euro bilioni 5.6 zaidi ifikapo mwaka 2014 bila ya kutaja ni katika maeneo gani mikasi itapitishwa.
Kansela Merkel ameonya hapo kabla kuwa kubana matumizi katika bajeti ya serikali ya shirikisho itakuwa jambo la kihistoria kwa ajili ya Ujerumani mpya, nchi iliyoundwa mwaka 1949.
Serikali ya muungano ya vyama vitatu iliyoundwa na kansela Merkel ambayo ilikuwa inavutana, imeufahamisha umma wa nchi hiyo katikati ya mwezi Mei kuwa mikasi mikubwa haiepukiki. Wafanyakazi wa serikali huenda pia wakapitiwa na panga hilo na kupoteza kazi zao na Wajerumani huenda wakapoteza haki ya kupunguza aina fulani ya matumizi kutoka katika kodi yao ya mapato.
Baraza hilo la mawaziri hata hivyo limepinga wazo la kupandisha viwango vya kodi ya mapato. Merkel ameeleza wazi , kuwa hakutakuwa na mabadiliko katika kodi ya ongezeko la thamani, kwa ajili ya vyakula ama masuala ya kitamaduni. Wananchi hawana haja ya kutia wasi wasi , kwamba katika maeneo haya kutafanyika mabadiliko.
Kansela Angela Merkel amesema kuwa mabadiliko yatalikumba pia jeshi la ulinzi. Merkel hakueleza mabadiliko hayo katika jeshi la ulinzi mara moja, lakini amesema kuwa hayatakuwa madogo.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, ambaye ni makamu wa kansela Guido Westerwelle na kiongozi wa chama cha FDP kinachounda serikali ya mseto pamoja na chama cha kansela Merkel , amesema kuwa punguzo kwa mwaka ujao pekee litafikia kiasi cha Euro bilioni 11.1.
Mwandishi: Sekione Kitojo/ DPAE/DPA
Mhariri : Othman Miraj.