1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la mawaziri Kenya laanza rasmi mapumziko ya siku 10

17 Agosti 2020

Baraza la mawaziri linaanza rasmi mapumziko ya siku 10 Kama alivyoagiza raise Uhuru Kenyatta. Hatua hiyo imezua hisia mseto na kusukuma hoja kuwa mabadiliko yananukia kwenye Baraza la mawaziri.

https://p.dw.com/p/3h4Zx
Kenia Symbolbild Wahlen und Social Media
Picha: AFP/T. Karumba

Agizo hilo la rais limezua hisia mseto kuwa huenda kiongozi wa taifa akatumia fursa hiyo kufanya mabadiliko kwenye baraza la mawaziri. Wanaoaminika kuwa karibu na rais wanaripotiwa kusema kuwa muda wa kufanya mageuzi hayo umewadia.

Kwa upande wa pili baadhi ya wandani wa kisiasa wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga wamekuwa wakielezea wasiwasi wao mintarafu maridhiano kati ya rais uhuru na jemedari wao. Viongozi hao wawili walifikia mwafaka kushirikiana mwezi Machi mwaka 2018, kwa kile kinachojulikana kama salamu za kheri, zilizosaidia kupunguza joto la kisiasa na mpasuko uliokuwepo kati ya Wakenya.

Hata hivyo, mkuu wa idara ya huduma za umma, Joseph Kinyua amepuuzilia mbali tetesi za kufanya mabadiliko kwenye Baraza la mawaziri. Badala yake anasisitiza kuwa kiongozi wa taifa ana imani na kikosi chake.

Duru zinaashiria kuwa rais huenda akawasogeza karibu wandani wake wa kisiasa ili kulipa nguvu mpya baraza la mawaziri. Inasadikika kuwa upande wa upinzani unatiwa shaka na hali ya kisiasa ukizingatia kuwa uchaguzi mkuu umepangwa kufanyika 2022. Vyama vya kisiasa tayari vimeanza maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao.

Saa chache zilizopita mkuu wa idara ya huduma za umma Joseph Kinyua ameweka bayana kuwa mawaziri hawatakuwa na majukumu yoyote wakati huu wa mapumziko. Mapumziko hayo yatafikia kikomo tarehe 28 mwezi huu wa Agosti.