1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BARAZA LA KIJAMII LAFUNGULIWA BRAZIL

Mohamed Dahman27 Januari 2005

Kikao cha Baraza la Tano la Kijamii Duniani kimeanza hapo Jumaatano katika mji ulioko kusini mwa Brazil wa Porto Alegre na kurudi katika mahala kulikozaliwa mkutano huu mkubwa kabisa wa jamii ya kiraia unaofanyika kila mwaka.

https://p.dw.com/p/CHhc
Polisi wakiwa katika Kikao cha Baraza la Kijamii mjini Mumbai India mwaka 2004
Polisi wakiwa katika Kikao cha Baraza la Kijamii mjini Mumbai India mwaka 2004Picha: AP

Lakini safari hii watayarishaji wamekunjuwa utaratibu mpya wa kuwa na utulivu na nidhamu badala ya vurugu wakati takriban washiriki 120,000 wakiwa tayari kwa siku tano za mikutano warsha na mijadala ya majopo juu ya masuala mbali mbali kuanzia madeni,umaskini na maendeleo.

Salete Valesan wa Brazil,Meena Menon wa India na Njoroge Njehu wa Kenya walizungumza na waandishi wa habari juu ya dhana mbali mbali za utaratibu uliopitishwa kwa ajili ya Baraza la Kijamii Duniani katika kikao chake cha mwaka 2005.

Waziri wa serikali ya Brazil Luiz Dulci alihudhuria mkutano huo wa waandishi wa habari akiwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Luiz Inacio Lula da Silva na alitumia fursa hiyo kuelezea mchango wa Baraza la Kijamii Duniani kuifanya jamii ya kiraia kuwa nguvu ambayo kila serikali duniani inabidi iizingatie.

Waziri huyo aliuliza iwapo kuna uwezekano wa kuwa na dunia aina nyengine akifafanuwa mada ya mkutano huo wa kila mwaka na kuendelea kusema dunia hiyo nyengine tayari iko njiani inakuja na tayari inajengwa.

Mikutano minne iliopita ya baraza hilo ambapo mitatu ya kwanza ilifanyika katika mji wa Porto Alegre wakati ule wa mwaka 2004 ulifanyika mjini Mumbai India haikujishughulisha na mijadala tu bali pia tafakuri ya pamoja na haikuwa kwa ajili ya kubadilisha mawazo tu bali pia uzoefu wa hali ya juu wa vitendo mambo ambayo waziri Luis anasema yanapaswa kuagaliwa na serikali zote duniani.

Waziri huyo alimalizia kwa kuzungumzia mada ya serikali kugharamia Baraza la Kijamii Duniani kwa kusema hakuna kitu cha kufurahisha zaidi kuliko msaada wa serikali kwa jamii hususan pale serikali inapoheshimu uhuru wa kisiasa na kitamaduni wa baraza hilo.

Wakati huo huo Valesan ameweka nadhari kwa utaratibu mpya ambao ulikubaliwa hapo mwaka 2004 kwa ajili ya mkutano wa mwaka huu wa Baraza la Kijamii Duniani ambapo katika miaka iliopita uliwakusanya wataalamu na wanaharakati wa jamii ya kiraia kutoka fani mbali mbali na kutoka katika kila pembe ya dunia.

Kwa upande wake Menon msemaji wa kike wa Baraza la Kijamii kwa mwaka 2004 lililofanyika mjini Mumbai anasema nchi yake inathamini sana vuguguvu hili lililozaliwa miaka mitano iliopita katika mji wa Porto Alegre.

Menon amekaririwa akisema vuguvugu lililoanza hapo lilikuwa muhimu sana hususan kwa India na bara la Asia kwa ujumla kwa kuwapa mtizamo mpya katika mapambano dhidi ya vita na njaa.

Kikao kijacho cha Baraza la Kijamii Duniani ambalo litakuwa baraza litakalofanyika kimataifa kwa wakati mmoja Barani Afrika, Asia,Marekani na Ulaya litakuwa fursa adhimu kabisa kwa mabara manne kufikisha ujumbe wa bazara hilo.

Mwakilishi wa Kenya Njehu ambaye anashiriki katika jopo kwa sababu Baraza la Kijamii kwa mwaka 2007 litafanyika Afrika anasisitiza kwamba Porto Alegre ni maskani ya kwanza kuwa kuwahi nayo jamii ya kiraia.

Mwanaharakati huyo anasema mustakbali upo hapo lakini pia ni muhimu kuangalia mbele na kuongeza kusema hata hivyo safari haitokuwa rahisi na kwamba vita dhidi ya sera za Shirika la Fedha la Kimataifa,Benki ya Dunia na Shirika la Biashara Duniani vitaendelea.Amezishutumu taasisi hizo kwa kupitisha hatua zenye kuwaumiza Waafrika walio maskini kabisa.

Mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Adolfo Perez Esquivel wa Argentina kwa upande wake ametowa wito wa kufutwa bila ya masharti kwa madeni ya kigeni kwa nchi za kimaskini.Amesema madeni hayo kwa nchi hizo za kimaskini ni mauaji ya halaiki ya kijamii na kufutwa kwake ni jambo lenye umuhimu wa dharura.

Zaidi ya wanaharakati 50,000 wanaopinga utandawazi hapo Jumaatano walijimwaga katika mitaa ya Porto Alegre katika maandamao yaliokusudia kupinga mkutano wa viongozi wa Davos wa viogogo vya kisiasa,fedha na uchumi duniani.

Mkusanyiko huo wa kusisimuwa wa wanaharakati wa kupinga vita,wanamazingira,wapigania uhuru wa kutowa mawazo na kutenda,wanaharakati wa vyama vya wafanyakazi na wanamgambo wanaopinga serikali umepangwa kwenda sambamba na mkutano mpinzani wake Baraza la Kiuchumi Duniani unaofanyika mbali maelfu ya kilomita katika makao maridadi ya mapumziko ya watalii ya Davos katika milima ya Uswisi.