Baraza la Katiba Senegal lafuta uamuzi kuahirisha uchaguzi
16 Februari 2024Uamuzi huo wa kihistoria unazidisha suintafahamu katika taifa hilo la Afrika Magharibi ambalo kijadi limekuwa na utulivu.
Baraza hilo la Katiba limesema muswada uliopitishwa na bunge wa kuchelewesha uchaguzi ulikuwa kinyume na katiba, kulingana na nyaraka iliyothibitishwa na chanzo kimoja ndani ya taasisi hiyo.
Baraza hilo pia liliwahi kubatilisha agizo la Rais Macky Sallla Februari 3 ambalo lilikuwa limebadilisha ratiba ya uchaguzi wiki tatu tu kabla ya kupiga kura.
Soma zaidi: Wabunge wakamatwa wakipinga kuahirishwa uchaguzi Senegal
Uamuzi wa kuchelewesha uchaguzi, ambao awali ulikuwa ufanyike Februari 25, umeitumbukiza Senegal katika mzozo mbaya wa kisiasa na kuchochea hasira ya umma na maandamano ya vurugu.
Upinzani na makundi ya asasi za kiraia yalikuwa yameitisha maandamano mapya siku ya Ijumaa (Februari 16) .