1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Haki za Binadamu chombo pekee kutetea haki hizo

P.Martin8 Mei 2007

Kwa mujibu wa makundi mawili yanayotetea haki za binadamu,Angola,Belarus,Misri na Qatar hazifai kuwa wanachama katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/CHEj

Nchi hizo nne ni miongoni mwa mataifa 15 yanayogombea viti 14 katika Baraza la Haki za Binadamu,ambalo mwaka jana lilichukua nafasi ya Halmashauri ya Haki za Binadamu iliyopteza sifa. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litachagua wanachama wapya tarehe 17 mwezi huu.Ripoti kuhusu mwaka wa kwanza wa baraza hilo jipya,iliyotolewa na kundi mojawapo linalogombea haki za binadamu, “UN Watch” inasema,baraza jipya si bora zaidi ya mtangulizi wake,likishughulika zaidi kuilani Israel.

Kwa upande mwingine,kundi la “Human Rights Watch” lenye makao yake mjini New York,limeihimiza Marekani kupeleka mjumbe wa kudumu katika baraza hilo,lakini hadi hivi sasa,Marekani imekataa kugombea uanachama.Mkurugenzi mtendaji wa kundi hilo,bwana Kenneth Roth,katika barua aliyopeleka kwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani,Bibi Condoleezza Rice amesema,licha ya kasoro zake, baraza hilo ni jukwaa muhimu la kimataifa kulinda haki za binadamu na misingi ya uhuru.Hakuna chombo kingine kinachotetea haki hizo.

Wakati huo huo,ripoti ya pamoja iliyotolewa siku ya Jumatatu na makundi mawili yanayogombea haki za binadamu,yaani “UN Watch” na “Freedom House” imesema,Angola,Belarus,Misri na Qatar ni nchi zenye utawala wa kiimla na vile vile zimekiuka haki za binadamu.Hata katika Umoja wa Mataifa, nchi hizo nne zimepiga kura kupinga masuala yaliyohusika na haki za binadamu na hivyo kwa maoni ya makundi hayo mawili,nchi hizo hazistahili kuwa wanachama katika Baraza la Haki za Binadamu lililo na makao yake mjini Geneva. Mwaka huu,baraza hilo lenye viti 47,lina nafasi 14 tu zilizo tupu.Belarus na Slovenia zinagombea viti viwili vya Ulaya ya Mashariki.Naibu mkurugenzi mtendaji wa “Freedom House” amesema, nchi za magharibi zikijaribu kuipiga kumbo Belarus,zimeitaka Bosnia igombee kiti katika baraza hilo,lakini wanadiplomasia wamesema, Slovenia imetishia kujitoa ikiwa Bosnia itajiingiza katika kinyanganyiro hicho.Marekani na Umoja wa Ulaya,tangu muda mrefu zinamtuhumu Rais Alexander Lukashenko wa Belarus kuwa anakandamiza kila aina ya upinzani na kukaba vyombo vya habari.India,Indonesia,Uholanzi, Ufilipino na Afrika ya Kusini ni wanachama wanaogombea kuchaguliwa tena.Baraza hili jipya liliundwa baada ya aliekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Kofi Annan kusema halmashauri ya hapo awali ilipoteza uaminifu vibaya sana,hadi kuathiri kwa jumla sifa ya Umoja wa Mataifa. Halmashauri hiyo,imetuhumiwa vikali na nchi za magharibi kuwa ilipuuza ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi zinazoendelea.