1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Umoja wa Mataifa wajadili uhalifu wa Urusi nchini Ukraine

27 Februari 2023

Zaidi ya wakuu 100 wa nchi pamoja na mawaziri wanashiriki kikao cha Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa kuanzia leo kujadili masuala kadhaa hususan ya uhalifu wa kivita nchini Urusi.

https://p.dw.com/p/4O16e
Internationale Proteste zum Jahrestag des Ukraine Kriegs
Picha: Georgi Paleykov/NurPhoto/IMAGO

Zaidi ya wakuu 100 wa nchi pamoja na mawaziri watashiriki kikao cha Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa kinachofanyika mjini Geneva, Uswisi kuanzia leo Jumatatu wakiangazia namna ya kukabiliana na masuala kadha, kuanzia madai ya Urusi kufanya uhalifu wa kivita nchini Ukraine hadi namna China inavyowatendea Waislamu wa jamii ya walio wachache wa Uyghur. 

Kwenye kikao hicho, ambacho kinafunguliwa hii leo na kuendele hadi Aprili 4, mataifa hayo yatakuwa na fursa ya kujadiliana kuhusu kukiongezea muda chombo cha Umoja wa Mataifa kilichoundwa kufanya uchunguzi wa madai ya mauaji ya kiholela nchini Ukraine.

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Ryabkov anatarajiwa kuhutubia kikao hicho siku ya Alhamisi. Atakuwa afisa wa kwnaza wa Moscow kukutana na viongozi wenzake ana kwa ana tangu taifa hilo lilipoivamia Ukraine mwaka mmoja uliopita. Urusi inayokana kufanya uhalifu huo wa kivita ama kuwalenga raia nchini Ukraine, ilisimamishwa kwenye baraza hilo kufuatia uvamizi wake mwezi Aprili mwaka jana, lakini bado inaruhusiwa tu kushiriki kama mwangalizi.

Sergei Alexejewitsch Rjabkow | stellvertretender russischer Außenminister
Naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Ryabkov, atahutubia BAraza hilo safari hii kwa mara ya kwanza tangu taifa hilo lilipoivamia Ukraine.Picha: Joe Klamar/AFP/Getty Images

Wanadiplomasia wa magharibi wamekuwa kimya kuzungumzia uwepo wa naibu waziri huyo na hasa baada ya kususia hotuba ya waziri wa mambo ya nje Sergei Lavrov aliyoitoa kwenye baraza hilo mwaka jana kuhusiana na hatua yake ya kuivamia Ukraine.

Huko Kyiv kwenyewe, rais Volodymyr Zelensky amemfuta kazi afisa wa ngazi za juu wa jeshi katika mkoa wa Donbass, ingawa hakukutolewa sababu ya kufutwa kwake. Amri ya kufutwa kwake ilisema Eduard Moskalyov hataendelea kuwa kamanda wa vikosi vya muungano. Alikuwa akishikilia wadhifa huo tangu Machi mwaka jana.

Soma Zaidi: Ukraine yatoa heshima kwa wanajeshi waliopoteza maisha

Kumesikika ving'ora vya tahadhari usiku mzima wa jana katika mji mkuu wa Kyiv na majiji mengine na kumeripotiwa kifo cha mtu mmoja kufuatia mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Urusi katika mji mmoja ulioko magharibi mwa nchi hiyo, hii ikiwa ni kulingana na meya wa eneo hilo kupitia ujumbe wake wa Telegram.

Katika hatua nyingine, Marekani imeionya China kwamba itakabiliwa na hatua kali iwapo itaisaidia Urusi kisilaha. Hofu ya mataifa ya magharibi juu ya msaada wa kijeshi wa China, inajitokeza wakati Urusi inahangaika kufanikisha azma yake ya uvamizi nchini Ukraine, lakini kwa upande mwingine, jirani yake huyo naye akijiandaa na mashambulizi ya kushtukiza kwa kutumia silaha za kisasa zaidi ilizopewa na washirika wa magharibi, ikiwa ni pamoja na vifaru vya kivita.

Beijing imekataa katakata kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na badala yake ikatoa mapendekezo ya kupatikana kwa suluhu kwa njia ya amani wakati wa maadhimisho ya mwaka mmoja wa vita hivyo. Hata hivyo mapendekezo hayo yalipokelewa kwa mashaka makubwa na Ukraine yeyewe, wafuatiliaji na hata mataifa ya magharibi hasa kutokana na ukaribu uliopo baina ya Urusi na China.