Barack Obama ziarani Berlin
18 Juni 2013Tunaanza na ziara ya rais wa Marekani Barack Obama mjini Berlin,gazeti la Mittelbayerische Zeitung linaandika:"Nusu karne baada ya ziara ya John F.Kennedy,kinachohitajika hivi sasa sio tena kusifiana bali ufumbuzi thabiti wa matatizo yaliyopo.Kuanzia kuzorota ukuaji wa kiuchumi na mgogoro wa sarafu ya euro,kupitia Syria,Iran na Korea ya kaskazini hadi kufikia masuala ya nishati na kuhifadhiwa data za watu.Washirika wanakutana mjini Berlin wakiwa katika hali ya usawa.Jambo ambalo ni muhimu kwa ulimwengu na pia kwa Ulaya.
Gazeti la "Der neue Tag linazungumzia kuhusu makubaliano ya soko huru kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya.Gazeti linaendelea kuandika:"Kutangazwa tarehe ya kuanza mazungumzo kati ya Umoja wa ulaya na Marekani kuhusu makubaliano ya soko huru ni ishara njema.Soko hilo litazifaidisha pande zote mbili.Kwasababu biashara huru kati ya madola yaliyoendelea sana kiuchumi inafungua milango ya neema kwa wote wanaohusika.Na ukuaji wa kiuchumi,wanahitaji haraka tangu wamarekani mpaka wakaazi wa Ulaya.
Kwanini walimwengu wanakaa kimya?
Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamemulika pia hali nchini Uturuki na kukosoa jinsi walimwengu wanavyofanya tahadhari.Gazeti la "Sächsische Zeitung" linaandika:Tahadhari za walimwengu katika kuikosoa Uturuki zinamaanisha kitu kimoja tu na kinahusu umuhimu wa kimkakati wa Uturuki.Hakuna anaetaka kutamka maneno makali kwa kuhofia yasije yakachochea mivutano ya kisiasa na kuitenga Ankara.Erdogan bado ana turufu mkononi:Wazungu na wamarekani wana msimamo wa ndumila kuwili.Kwa nchi za Umoja wa ulaya,halizuki suala angalao kwa sasa la kuichukulia Uturuki kama mshirika-seuze mwanachama kamili.Kwanini lakini nchi hiyo,inaendelea kuwa mshirika katika jumuia ya kujihami ya NATO licha ya matumizi yaliyokithiri ya nguvu dhidi ya waandamanaji"Hakuna aliyeweza kutoa jibu la kuridhisha la suala hilo hadi sasa.
.SPD watapa tapa
Mada yetu ya mwisho magazeti inamulika mivutano ndani ya chama cha upinzani cha Social Democratic SPD,miezi mitatu kabla ya uchaguzi mkuu.Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linaandika:"Peer Steinbrück na SPD wana chini ya siku 100 kuugeuza mkondo wa mambo:Kila kitu kinaashiria hawatofanikiwa-hata kama SPD sasa wanaanza kuzindukana na kusimama kidete nyuma ya uongozi wao.Steinbrück anatambua fika kitakachojiri pindi SPD wakishindwa katika uchaguzi mkuu ujao.Atakaeshindwa zaidi ni yeye mwenyewe.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman