Barabara ya kuelekea Brazil 2014
18 Juni 2013Misri, Ethiopia, Cote d'Ivoire, Tunisia, na Algeria ndio nchi za kwanza barani Afrika kuingia katika awamu ya mchujo ya mechi za kufuzu katika dimba la kombe la dunia litakaloandaliwa nchini Brazil hapo mwakani. Hata hivyo taarifa iliyotolewa na shirikisho la soka ulimwenguni FIFA baada ya mechi hizo za mwishoni mwa wiki, imesema wanachunguza madai kwamba Ethiopia, Guinea ya Ikweta na Togo waliwatumia wachezaji ambao hawakustahili kucheza katika mechi za mwaka huu za kufuzu. Nchi itakayopatikana na hatia wakati wa awamu ya kufuzu barani Afrika itanyimwa pointi itakazopata na kupewa wapinzani wao ushindi wa mabao matatu kwa sifuri.
Ushindi wa Ethiopia wa magoli mawili kwa moja dhidi ya Botswana, na ushindi wa mabao mawili kwa sifuri wa Togo nyumbani dhidi ya Cameroon katika mwezi wa Juni, na ushindi wa nyumbani wa magoli manne kwa matatu wa Guinea ya Ikweta dhidi ya Visiwa vya Cape Verde mittau iliyopita unachunguzwa. Kama Ethiopia watapoteza pointi tatu, hawatakuwa na uhakika wa kushinda katika kundi A, kama Togo watapokonywa pointi tatu, Cameroon watachukua nafasi ya Libya kama viongozi wa kundi I, na kama Guinea ya Ikweta itapokonywa tatu, Tunisia itakuwa na uhakika wa kuwa viongozi wa kundi B.
Katika matokeo ya karibuni, Ethiopia waliwazaba Afrika Kusini mabao mawili kwa moja na sasa wanaongoza kundi A na pengo la pointi tano ikisalia awamu moja pekee. Misri walipata ushindi wa goli moja kwa sifuri dhidi ya Msumbiji mjini Maputo na kuweka uongozi wa pengo la pointi tano mbele ya Guinea katika kundi G.
Cote d'Ivoire waliifunga Tanzania mabao manne kwa mawili jijini Dar es Salaam na kuchukua uongozi wa kundi C ambao hawawezi kamwe kupokonywa. Tunisia walihitaji pointi moja ugenini dhidi ya Guinea ya Ikweta na kupata uongozi wa kundi B. baada ya kushinda moja kwa sifuri dhidi ya Rwanda, Algeria walilazimika kusubiri kabla ya mali kukabwa sare ya mabao mawili kwa mawili na Benin. Ghana waliwafunga Lesotho mabao mawili kwa sifuri na sasa wako mbele ya Zambia katika kundi D.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman