Bandari na uwanja wa ndege Yemen kufunguliwa tena
23 Novemba 2017Muungano huo umesema utaifungua bandari ya Hodeida kupokea vifaa muhimu vya misaada vinavyohitajika kwa haraka na uwanja wa ndege wa Sanaa kwa ndege za Umoja wa Mataifa mchana wa alkhamisi.
Haukutaja wakati au kama ungeweza kuondoa hatua ya kuzuia safari za meli za kibiashara kutoka na kuingia Yemen.
Hodeida, mji ambao unadhibitiwa na waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran - mpinzani mkuu wa Saudi Arabia, ni njia muhimu ya bidhaa za chakula na madawa zinazohitajika sana Yemen.
Muungano huo uliweka kizuizi cha bandari za Yemen na viwanja vya ndege siku mbili baada ya Wahouthi kufyetua kombora kwenye ardhi ya Saudi Arabia mnamo Novemba 4.
Kombora hilo lilizuiwa karibu na uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mfalme Khalid mjini Riyadh, na kusababisha vita vya maneno kati ya Iran na Saudia Arabia, ambayo ililaumu Iran kwa "ukatili wa moja kwa moja" na kwa kuwapa silaha kwa waHouthi.
Umoja wa Mataifa ulisema siku ya Jumatano kuwa ulijulishwa na Saudi Arabia juu ya uamuzi wa kuzifungua tena bandari za Yemeni za Hodeida na Saleef, pamoja na uwanja wa ndege wa mji mkuu Sanaa.
"Tunafuatilia maendeleo haya na kujaribu kuona ikiwa kweli yatafanyika, "msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq aliwaambia waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja huo mjini New York."
"Bila shaka, kama hilo likitokea itakua hatua ya maendeleo ,ya kukubalika na muhimu sana."
Shirika la Msaada la Save the Children liliupongeza uamuzi wa muungano huo lakini lilisema ufunguzi wa bandari na uwanja wa ndege hautatoshi kukabiliana na ukame unaoweza kutokea nchini Yemen".
Misaada ya kibinadamu inatoa tu sehemu ndogo ya bidhaa muhimu zinazohitajika Yemen - vifaa vya kibiashara ni muhimu kulisha idadi ya watu na kuhakikisha huduma za msingi zinaendelea kupatikana," alisema.
Mkuu wa misaada ya Umoja wa Mataifa Mark Lowcock aliomba vikwazo hivyo viondolewe mnamo Novemba 8, akionya kuwa Yemen ingeweza kukabiliwa na "baa kubwa la njaa ulimwenguni kwa miaka mingi"
Serikali ya wahouthi mnamo siku ya jumanne ilitangaza kwamba uwanja mkuu wa ndege wa kimataifa unafanya kazi tena wiki moja baada ya shambulizi la muungano wa kijeshi unaongozwa na Saudia kuuharibu mtambo wa kuongoza safari za ndege.
Uwanja huo wa ndege ulikuwa wazi tu kwa ajili ya ndege zinazopeleka msaada wa kibinadamu.
Wakishirikiana na rais wa zamani Ali Abdullah Saleh, waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran wanadhibiti mji mkuu wa Sanaa pamoja na maeneo ya Yemen Kaskazini.
Mnamo mwaka wa 2015, Saudia Arabia na washirika wake walijiunga na mapigano ya serikali ya Yemen dhidi ya waasi hao.
Zaidi ya watu 8750 wameuawa.
Taifa hilo pia linakabiliwa na mlipuko wa kipindupindu na mamilioni wanakabiliwa na hatari ya kukumbwa na ukame.
Mwandishi: Fathiya Omar/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef