Ban Ki Moon kuzungumza na viongozi wa Afrika kuhusu Zimbabwe
20 Aprili 2008HARARE
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Kimoon amesema atajadiliana na viongozi kadhaa wa Afrika kuhusu mgogoro wa Zimbabwe katika mkutano wa Umoja wa mataifa kuhusu masuala ya kibiashara na maendeleo unaoanza leo nchini Ghana.Matamshi hayo ya Ban Ki Moon yamekuwa baada ya hapo jana katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa mataifa Kofi Annan kuwatolea mwito viongozi wa Afrika kuingilia kati kwa haraka na kuutatua mgogoro juu ya uchaguzi wa Zimbabwe.Kofi Annan ameonya kwamba hali inayoendelea Zimbabwe inatishia usalama hata katika nchi jirani.
Maafisa wa uchaguzi nchini humo hapo jana walianza zoezi la kuhesabu tena kura za urais za uchaguzi wa marchi 29 licha upinzani kufanya juhudi za kupinga zoezi hilo na hofu iliyoenea kwamba mvutano huu wa kisiasa huenda ukaibua ghasia.
Kiongozi wa upinzani wa chama cha Movement foer Demokratic Change MDC Morgan Tsvangirai ambaye yuko nchini Afrika kusini amesema anahofia kushambuliwa au kutiwa nguvuni endapo atarudi nchini Zimbabwe.Zoezi hilo la kuhesabu tena kura huenda likayabadilisha matokeo ya mwanzo ya uchaguzi wa bunge ambayo yalionyesha kuwa chama cha rais Robert Zanu pf kilikuwa kimepoteza wingi wa viti bungeni.Maafisa wa tume ya uchaguzi wamesema zozei hilo la kuhesabu tena kura katika maeneo bunge 23 litachukua muda wa siku tatu.Wakati huohuo meli ya China iliyobeba shehena ya silaha za kupelekwa Zimbabwe inasemekana kuelekea Angola kuteremsha shehena hiyo baada ya kukataliwa kufanya hivyo kupitia Afrika Kusini.