Ban Ki-moon ashutumu matumizi ya silaha za sumu Syria
14 Desemba 2013Ban ameliambia baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuwa jumuiya ya kimataifa pia ina wajibu wa kimaadili na wajibu wa kisiasa kuzuwia matukio zaidi na kuhakikisha kuwa silaha za sumu hazitatumika tena kama zana za kivita.
Amelihutubia baraza hilo kuu lenye wanachama 193 kuhusiana na ripoti ya mwisho iliyotolewa siku ya Alhamis na wakaguzi wa Umoja wa Mataifa ambao walikagua maeneo kulikofanywa mashambulio saba ya silaha za sumu nchini Syria.
Taarifa yao imeeleza kuwa silaha za sumu huenda zilitumika katika maeneo manne, pamoja na shambulio lililothibitishwa karibu na mji mkuu Damascus mwezi Agosti ambalo liliilazimisha serikali ya nchi hiyo kuamua kuteketeza hazina yake ya silaha za sumu.
Mamlaka maalum ya wakaguzi hao yaliwapa mamlaka ya kutoa maelezo iwapo silaha hizo za sumu zilitumika lakini hawakutakiwa kusema iwapo serikali ama wapiganaji wa upinzani wanahusika na shambulio lolote kati ya hayo.
Muungano wa kitaifa wa upinzani katika taarifa umesema mashambulio hayo yamefanywa na utawala wa rais Assad na kusema ripoti hiyo inapaswa kuimarisha nia ya jumuiya ya kimataifa kuiweka serikali ya Syria kuwa ndio inayohusika na mashambulio hayo.
Hatua zinahitajika haraka
"Ushahidi umeonesha mara kadha kuwa utawala wa rais Assad umetumia silaha za sumu dhidi ya watu wa Syria. Hatua za haraka kwa hiyo zinahitajika kuchukuliwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuipeleka Syria katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita na kuhakikisha kuwa wanaohusika na mashambulio hayo wanafikishwa mbele ya sheria," amesema Dr. Najib Ghadbian, mwakilishi wa kundi hilo.
Lakini mkuu wa wakaguzi wa Umoja wa Mataifa Ake Sellstrom amewaambia waandishi habari kuwa "mbinu za ndani zaidi" kuliko zili zilizoidhinishwa na baraza kuu kwa ukaguzi wao zinahitajika ili kuwataja wahusika wa mashambulio hayo.
"Naweza kutabiri ... lakini sina taarifa ambazo zitasaidia mahakamani," amesema. Sellstrom amesema kuwa mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa wanaweza kuidhinisha uchunguzi mwingine wa kina wa alama katika eneo la tukio" kutambua wale waliohusika, hali ambayo itahitaji gharama zaidi na matumizi ya mbinu ambazo kikosi chake hakikutumia. Hakufafanua.
Uchunguzi zaidi wahitajika
Mkuu wa taasisi ya upunguzaji wa silaha wa Umoja wa mataifa Angela Kane amewaambia waandishi habari kuwa kuna idadi kadha ya miito ya kufanyika uchunguzi zaidi kutambua wale ambao wanahusika na mashambulio hayo ya silaha za sumu.
Tume iliyoundwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa tayari imeamua kuwa pande zote mbili zimefanya uhalifu wa kivita wakati wa mzozo huo.
Tume hiyo yenye makao yake makuu mjini Geneva inatayarisha orodha ya siri ya watuhumiwa wa uhalifu, ambayo imehifadhiwa na kamishna wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay, na inatarajiwa hatimaye kupima nani hasa anawajibika na mashambulio hayo ya silaha za sumu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri : Bruce Amani