1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Balozi wa Marekani nchini Libya auawa

12 Septemba 2012

Balozi wa Marekani nchini Libya na wafanyakazi wengine wa ubalozi huo wameuawa kutokana na mashambulizi ya roketi katika mji wa Benghazi yanayohusishwa na maandamano ya Waislamu kupinga filamu inayomkashifu Mtume wao.

https://p.dw.com/p/167CT
Mashambulizi dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Benghazi, Libya.
Mashambulizi dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Benghazi, Libya.Picha: Reuters

Afisa mmoja wa serikali ya Libya amethibitisha kwamba Balozi Chriss Stevens na wafanyakazi wengine watatu wa ubalozi huo waliuawa kwa roketi lililorushwa kwenye gari ya ubalozi. Hata hivyo, haikubainika mara moja kama balozi huyo alikuwamo kwenye gari iliyoshambuliwa, au alikufa usiku wa kuamkia leo, baada ya waandamanaji wenye silaha kuuvamia ubalozi huo mjini Benghazi.

Waandamanaji hao walikuwa wamekasirishwa na filamu moja ya Hollywood ambayo inayakashifu kiongozi wa Waislamu, Mtume Muhammad. Maandamano kama hayo pia yalifanyika mjini Cairo, Misri, ambako maelfu ya waandamanaji waliuvamia ubalozi wa Marekani, lakini bila kuwapo visa vya mashambulizi. Wakristo wa madhehebu ya Koptik nao wamekusudia kufanya maandamano kupinga filamu hiyo, wakisema kuwa ni matusi kwa imani za watu wote.

Romney apata mwanya

Mgombea wa urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican, Mitt Romney, amelitumia tukio hilo kuushambulia utawala wa Rais Obama kwa kuwa pamoja na waandamanaji wa Kiislamu wenye siasa kali na sio pamoja na Wamarekani.

Mashambulizi dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Benghazi, Libya.
Mashambulizi dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Benghazi, Libya.Picha: Reuters

"Nimefadhaishwa na mashambulizi dhidi ya ubalozi wetu nchini Libya na Misri na mauaji ya balozi wetu. Ni aibu kwa utawala wa Obama kutoa jawabu iliyotoa kwa kutokulaani mashambulizi kwenye balozi zetu bali kusimama upande wa waandamanaji." Alisema Romney.

Hata hivyo, mapema wizara ya mambo ya nje ilitoa tamko la kulaani vikali mashambulizi hayo. Waziri wa Mambo ya Nje, Hillary Clinton, alisema amezungumza na Rais Mohammed al-Magariaf wa Libya juu ya mashambulizi hayo na kwa pamoja wakakubaliana kuchukua hatua za haraka.

Filamu ya Kashfa

Filamu hiyo ambayo ndicho kitovu cha machafuko na maandamano hayo imeandaliwa na raia wa Marekani mwenye asili ya Israel ambaye anaueleza Uislamu kama kidonda ndugu na kumuonesha Mtume Muhammad (S.A.W) akilala na wanawake, kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na gazeti la Wall Street Journal la Marekani.

Rais wa Libya, Mohammed el-Magarief (katikati).
Rais wa Libya, Mohammed el-Magarief (katikati).Picha: Reuters

Awali, mjni Tripoli, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Libya, Wanish al Sharif, aliliambia shirika la habari la Ufaransa (AFP), kuwa ofisa mmoja wa Marekani aliuawa na mwengine kujeruhiwa wakiwa mikononi mwa waandamanaji huku wafanyakazi wengine wakiokolewa na wapo salama. Sharif alisema waandamanaji waliuvamia ubalozi huo wa Marekani na kuanza kurusha risasi hewani kabla ya kuingia ndani na kuanza kuwashambulia wafanyakazi.

Msemaji wa wizara hiyo, Abdelmonoem al-Horr, alisema guruneti lililorushwa kwenye ubalozi huo liliripuka kwenye bustani iliyoko karibu na ubalozi huo. Watu walioshuhudia tukio hilo wamesema wavamizi waliiteremsha bendera ya Marekani iliyokuwepo kwenye ubalozi huo na kisha kuanza kuuchoma moto ubalozi huo.

Mashambulizi dhidi ya ubalozi Libya na Misri

Raia mwengine aliyeshuhudia tukio hilo alisema waandamanaji waliokuwa na silaha wakiwemo Waislamu wenye itikadi kali wa kundi la Salafi walifunga barabara za mitaa inayoelekea kweye ubalozi huo.

Mashambulizi dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Benghazi, Libya.
Mashambulizi dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Benghazi, Libya.Picha: Reuters

Hata hivyo, maandamano hayo yamepingwa na Baraza kuu la Uongozi la Libya, ambalo katika taarifa yake limekiita kitendo hicho ni kiovu na kisichotarajiwa kutokea kwa ubalozi wa Marekani mjini Benghazi.

Tukio la maandamano nchini Libya linafuatia tukio kama hilo lililofanywa na waandamanaji mjini Cairo hapo jana ambapo waandamanaji wapatao 3,000, wengi wao wakiwa ni wa kundi la Salafi, walipoandamana kwenye ubalozi wa Marekani nchini humo kupinga filamu kama hiyo inayomkashifu Mtume Muhammad (S.A.W)

Mamia ya watu waliuzingira ubalozi wa Marekani na kisha mmoja wao kuiteremsha bendera ya marekani na kupandisha bendera yanye rangi nyeusi iliyo na alama ya kiislamu, na kisha kusema Mungu ni mmoja na Muhammad ni Mtume wa Mungu.

Mwandishi: Khatib Mjaja/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef