1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Balozi Gambari akutana na kiongozi wa upinzani Aung San Suu Kyi

Saumu Mwasimba30 Septemba 2007

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Ibrahim Gambari amekutana na kiongozi wa upinzani nchini Myanmar Aung San Suu Kyi aliyeko kwenye kifungo cha ndani ya nyumba huko mjini Yangon.

https://p.dw.com/p/CB0q
Kiongozi wa upinzani Aung San Suu Kyi mwenye umri wa miaka 62 amekuwa kifungoni kwa miaka 18 sasa
Kiongozi wa upinzani Aung San Suu Kyi mwenye umri wa miaka 62 amekuwa kifungoni kwa miaka 18 sasaPicha: AP

Gambari pia alikutana na viongozi wa utawala wa kijeshi jana usiku huko Naypyidaw kiasi kilomita 350 kaskazini mwa mji mkuu Yangon, katika mazungumzo yaliyolenga kuushawishi utawala huo kukomesha matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji wanaounga mkono Demokrasia.

Ziara ya Gambari inatarajiwa kuibadili hali ya mambo nchini Myanmar ingawa kuna wasiwasi ikiwa kweli utawala wa kijeshi utafuata maagizo ya jumuiya ya kimataifa waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Milliband anasema

’’Jumuiya nzima ya kimataifa inaunga mkono ziara ya balozi Gambari na ni lazima tuhakikishe kwamba utawala wa Myanmar unafahamu juu ya matokeo ya kuipinga jumuiya ya kimataifa.’’

Wakati huohuo mjumbe wa Japan pia ameenda Myanmar kwa ajili ya kuutolea wito utawala wa kijeshi ufanye uchunguzi wa kina juu ya kuuwawa kwa kupigwa risasi mwandishi habari raia wa Japan wakati wa maandamano ya kuipinga serikali mjini Yangon.Taarifa nyingine zinasema utawala wa Myanmar umekubali kuziruhusu meli za chakula cha msaada kuingia nchini mwake.Meli hizo zilikuwa zimezuiwa kuingia kwenye eneo la Mandalay wakati wa ghasia za serikali dhidi ya waandamanaji wanaoililia Demokrasia.Wiki mbili zilizopita kumekuwa na maandamano makubwa ya kuipinga serikali katika miji mikubwa ya nchi hiyo.