1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bajeti ya Ujerumani yaweka rekodi mpya

17 Machi 2010

<p>Mdahalo wa bajeti ya serikali kuu ya Ujerumani na ripoti ya mwakilishi wa majeshi bungeni ni baadhi ya habari zilizotawala safu za mbele katika magazeti ya Ujerumani leo Jumatano. EXPRESS linasema:<p>

https://p.dw.com/p/MUv4

"Serikali inaisifu bajeti yake kama ni kazi ya ustadi wakati upande wa upinzani inaitaja kuwa ni ya kubabaisha tu. Bajeti hiyo itasababisha deni jipya la Euro 80 elfu milioni - hakuna serikali yo yote iliyofikia kiwango kama hicho. Isitoshe deni la jumla la matumizi yote ya serikali ni zaidi ya Euro trilioni 1.6. Hapo ni dhahiri kuwa hakuna matumaini yo yote ya kupunguziwa kodi katika miaka ijayo. Kutamka vingine ni kuwavunga wapiga kura."

"Kuna sababu ya kushtuka, bajeti mpya inapovunja rekodi ya zamani kwa maradufu. Lakini wakati huu wa msukosuko wa kifedha kote duniani, watu wamezoea kukabiliwa na tarakimu kubwa kubwa laandika gazeti la HESSISCHE-NIEDERSÄCHSISCHE ALLGEMEINE na kuongezea:

"Lakini hiyo itabadilika upesi, Waziri wa Fedha Wolfgang Schäuble atakapowasilisha tathmini mpya ya malipo ya kodi katika mwezi wa Mei. Hapo Schäuble ataeleza vipi na wapi pa kupunguza matumizi. Kwa vile wakati huo, uchaguzi katika jimbo la North Rhine Westphalia utakuwa tayari umemalizika, basi ukweli utadhihirika."

Kwa maoni ya gazeti la  NÜRNBERGER NACHRICHTEN:

"Bajeti iliyowakilishwa bungeni kwanza kabisa ni hati ya Kansela Angela Merkel na muungano wake wa vyama vya CDU,CSU na FDP na hailezi ukweli wa  mambo. Wao wanafahamu vizuri kuwa bajeti inayodaiwa kuwa haitomuumiza yeyote ni vigumu kuaminiwa. Kwani hayo madeni yanayorundikana wakati huu, yatakuwa yakilipwa hata na kizazi kilicho katika shule za chekechea hivi sasa."

Tukipindukia mada nyingine gazeti la FLENSBURGER TAGEBLATT linaeleza juu ya ripoti iliyotolewa na mwakilishi wa majeshi bungeni Reinhold Robbe kuhusu hali halisi inayokutikana jeshini.Linasema:

"Mjumbe huyo anaelewa vizuri namna ilivyo jeshini kwani "anaelalia kitanda ndie ajuae kunguni wake."  Kwa hivyo, ripoti yake ya  mwisho inapaswa kutiwa maanani. Kwani mjumbe huyo hasa ameyapa kipaumbele matatazo yanayowazuia wanajeshi kutekeleza kazi zao ipasavyo. Ila hizo, zilikuwa zikikosolewa na Robbe tangu miaka mitano iliyopita, kwa hivyo hajakosea kuhamaki kwani hakuna marekebisho ya maana yaliyofanyika lamalizia FLENSBURGER TAGEBLATT.

Mwandishi: P.Martin/DPA

Mhariri: M.Abdul-Rahman