Bajeti ya Obama
26 Februari 2009Rais Barack Obama wa Marekani, anatazamiwa hivi punde kutangaza (bajeti) au mpango wake wa kwanza kabisa wa matumizi ya serikali yake kwa mwaka huu wa 2009 wenye nakisi ya kiasi cha dala Trilion 1.75.Isitoshe,anatarajiwa kuchambua mpango wake mkubwa kabisa wa kuustawisha uchumi wa Marekani na kurekebisha mfumo wa huduma za afya.
Mpango huo unajumuishas juhudi za Rais Obama za kuukomboa uchumi wa Marekani kutoka msukosuko wake mkubwa kabisa tangu ule wa miaka ya 1930,utafanya kasoro katika hazina ya serikali kupanda kwa kima kikubwa kabisa cha asili-mia cha pato zima la Taifa la Marekani tangu vita vya pili vya dunia.
Matumizi yanayokusudiwa yataingiza dala bilioni 200 kugharimia vita nchini Iraq na Afghanistan mnamo miezi 18 ijayo pamoja na kitita kikubwa kabisa cha dala bilioni 634,mfuko wa matumizi wa kipindi cha miaka 10 kugharimia mageuzi ya mfumo wa bima za afya ,shina la kampeni ya uichaguzi ya Rais Obama -hii ni kwa muujibu afisa wa utawala wake alivyosema.
Isitoshe, Rais Obama ameomba kitita kingine cha dala bilioni 250 kukwekwa kando akiba ili kuyaokoa mabenki ya Marekani,mbali na kitita cha dala bilioni 700 kilichokwishatolewa kwa azma kama hiyo.
Serikali ya Obama kwa sasa haina azma ya kutumia kitita hicho, lakini ni akiba tu endapo ikihitajika-alisema afisa huyo.
"Halkadhalika, atakapotangaza bajeti yake Bungeni leo ,Rais Obama anatarajiwa kuzungumzia haja ya kutia raslimali katika sekta za nishati,elimu n a afya ili kuujenga uchumi wakati huo huo kuiweka Marekani katika mkondo wa kuujenga upya uchumi wake ,mkondo pekee madhubuti na wa uhakika kuweza kukua kwa muda mrefu na kustawisha maisha."ilisema taarifa ya Ikulu huko Washington.
Isitoshe, Rais Obama atalitaka Bunge kuidhinisha kitita cha dala bilioni 634 kugharimia huduma za afya wakati wa bajeti yake ya mwaka ujao wa 2010.
Tangazo lake la leo litatuwama juu ya ahadi zake nyingi alizotoa wakati wa kampeni yake ya uchaguzi wa rais na litakuwa ushahidi bora kabisa kushadidia hoja za Obama kuwa enzi ya msukosuko huu mkubwa kabisa wa kiuchumi ni fursa barabara ya kupitisha ufagio kufanya mageuzi makubwa ya kisiasa nchini.
Rais Barack Obama anatarajiwa pia kulitaka Bunge (Congress) kugharimia mageuzi katika sekta za elimu,nishati na mazingira na hivyo kutoa changamoto ya mabishano na chama cha Upinzani cha Republikan Bungeni .Hii itafuatia mabishano makali kati yao kuhusu mpango wake uliopitishwa karibuni wa kuustawisha uchumi ambao uliungwamkono na wabunge 3 tu wa chama hicho cha Upinzani.
Mwishoe, rais Obama atatimiza ahadi yake ya kampeni ya uchaguzi ya kuwapandishia kodi wamarekani wote wanavuna kima cha dala laki mbili unusu (250.000) kwa mwaka kutoka 35% na kukipandisha hadi 40%.Mpango huu utaingiza mapato katika hazina ya serikali kwa kima cha dala trilion 2mnamo miaka 10 ijayo.