1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bajeti ya EU bado ni suala tete

21 Februari 2020

Suala la bajeti ijayo ya Umoja wa Ulaya bado halijapatiwa ufumbuzi hata baada ya mazungumzo ya usiku kucha mjini Brussels.

https://p.dw.com/p/3Y7St
Brüssel | EU Gipfeltreffen
Viongozi wa Umoja wa Ulaya kwenye mkutano wa pamoja mjini BrusselsPicha: Reuters/R. Pareggiani

Mazungumzo kuhusu suala hilo tete yanatarajiwa kuanza tena leo wakati wa mkutano wa kilele unaotarajiwa kwenye makao makuu ya Umoja huo. 

Duru kutoka mjini Brussels zimearifu kuwa usiku wa kuamkia leo, rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel alifanya mazungumzo ya ana kwa ana na viongozi wote wakuu wa mataifa wanachama wa umoja huo lakini hakuna mpango wa pamoja ulioafikiwa kutatua mkwamo wa suala la bajeti.

Mashauriano mengine kama hayo yaliyopangwa kufanyika kwa pamoja na viongozi wote wa Umoja wa Ulaya asubuhi ya leo pia yameahirishwa kwa muda wa saa moja lakini vyanzo vimesema bado yatafanyika.

Vyanzo vya kidiplomasia viliashiria hapo kabla kuwa maafisa wakuu wa Umoja wa Ulaya wangefanikiwa kupitisha mpango wa bajeti utakaojadiliwa na viongozi wakuu wa nchi 27 za umoja huo wakati wa mkutano wa kilele unaofanyika leo.

Viongozi wa EU bado wamegawika 

Brüssel Präsident des Europäischen Rates Charles Michel Kanzlerin Merkel
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya Charles Michel akizungumza na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani mjini BrusselsPicha: Reuters/V. Mayo

Hata hivyo viongozi wa Umoja wa Ulaya kwa sehemu kubwa bado wamegawika juu ya kiwango cha fedha kinachopaswa kuidhinishwa kwa kipindi cha mwaka 2021 -2027 na kitakuwa na matokeo gani.

Michel aliwasilisha mapendekezo ya bajeti yenye thamani inayopindukia Euro Trilioni moja hatua iliyozusha ukosoaji kutoka pande tofauti.

Italia na Ureno zimesema haziwezi kuidhinisha mapendekezo hayo ya bajeti kutokana na hali dhaifu ya uchumi inayowakabili na mataifa mengi wanachama yanataka bajeti hiyo kupungua kwa hadi asilimia moja pekee ya pato jumla la Umoja wa Ulaya.

Mashauriano kuhusu bajeti ya Umoja wa Ulaya mara zote ni suala la mzozo ambalo huzusha migawanyiko kati ya mataifa wanachama yaliyo tajiri na yale masikini yanayotegemea kuata misaada na ruzuku.

Kwenye awamu hii, kuondoka kwa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya moja ya wachangiaji wakubwa wa bajeti ya umoja huu kumezidisha wasiwasi kwa kusababisha nakisi ya kati ya dola bilioni 65 hadi 81 ambazo zinapaswa kufidiwa kwa ama kupunguza matumizi au kutolewa michango zaidi na nchi wanachama.

Mataifa makubwa ya EU pia yanalalamika 

Brüssel | EU Gipfeltreffen: Emmanuel Macron spricht zur Presse
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa akizungumza na waandishi habari mjini BrusselsPicha: Reuters/Y. Herman

Wachangiaji wakuu Ujerumani, Austria, Uholanzi, Sweden na Denmark wanataka kupunguza kiwango wanachotoa wakisema wamekuwa wakichangia sehemu kubwa mno ya bajeti ya Umoja wa Ulaya.

Mataifa mengine wanachama yanapinga mapendekezo ya kupunguza matumizi wakishuku yataathiri kwa sehemu kubwa ruzuku muhimu katika sekta ya kilimo na fedha zinazotumika kuyasaidia mataifa masikini ya kanda ya umoja wa Ulaya.

Pamoja na hilo liko pia suala la malengo ya kisera ya Umoja wa Ulaya kwa miaka inayokuja ikiwemo dhamira ya kufikia viwango sifuri vya utoaji kesi ya Kbaoni ifikapo mwaka 2050.

Rais Emmanuel Macron ameonya dhidi ya Umoja wa Ulaya kufukia kichwa kwenye mchanga kwa madai ya kukosa fedha wakati unataka kufikia malengo iliyojiwekea.