Baiskeli zinazouzwa mnadani Ujerumani baada ya kuokotwa
3 Aprili 2024Shirika la Reli la Ujerumani la Deutsche Bahn limesema kuwa kila mwaka hupiga mnada mamia ya Baiskeli zilizosahaulika kwenye vituo vya treni.
Katika taarifa yake, shirika hilo la Deutsche Bahn limekadiria kuwa kila mwaka takribani baiskeli 2,700 hupatikana kwenye vituo vyake vipatavyo 5,400 vya treni zikiwa zimesahaulika na nusu ya baiskeli hizo hupigwa mnada baada ya kuzihifadhi kwa karibu wiki 10.
Gharama ya basikeli hizo hutofautiana kulingana na aina ya baiskeli na ubora wake, lakini kwa wastani mnada huo hugharimu kiasi cha euro 60 kwa baiskeli moja. Mnada huo pia unazihusisha baiskeli zinazotumia umeme maarufu kama e-bikes katika miji mbalimbali ya Ujerumani.
Soma: Dunia yaadhimisha siku ya kwanza ya baiskeli
Kulingana na taarifa ya shirika hilo, fedha zinazokusanywa kutokana na mauzo ya baiskeli hutumika katika usimamizi wa mali zilizopotea. Kiasi kikubwa cha mali zilizopotea na usimamizi wake kama vile uhifadhi, kurudisha kwa mmiliki na kuzichakata tena, hugharimu kiasi kikubwa cha pesa.
Kila mwaka, karibu vitu 250,000 hupotezwa na wasafiri katika vituo vya treni za masafa marefu na mitaani kote nchini Ujerumani. Vitu hivyo ni kama vile simu na kompyuta za mkononi yani Laptop. Kulingana na Deutsche Bahn, asilimia 60 ya vitu hivyo vinaweza kurudishwa kwa wamiliki wao, hasa bidhaa za thamani ya juu kama vile kompyuta za mkononi na simu.
Mtu yeyote aliyesahau baiskeli yake katika kituo chochote cha treni anaweza kuidai kwa kutoa uthibitisho wa baadhi ya sifa za mali yake kama vile ni baiskeli ya aina gani, rangi yake na wapi alikoisahau.Mwendesha baiskeli Froome atimiza ahadi yake
Kwa kawaida Ujerumani, yapo maeneo ya vitu vilivyopotea na kupatikana maarufu kama Lost and Found, ambapo kama umepoteza kifaa chako unaweza kwenda na kuulizia ili upatiwe.