BAIDOA:Wanajeshi wawili wa Ethiopia wauwawa kwenye shambulio la kujitoa muhanga
11 Oktoba 2007Mshambuliaji wa kujitoa muhanga alivurumiza gari alilokuwa akiliendesha katika kambi ya wanajeshi wa Ethiopia iliyoko nchini Somalia.
Wanajeshi wawili wameuwawa katika shambulio hilo ambalo linadhaniwa lililenga kumdhuru waziri mkuu wa Somalia Ali Mohamed Gedi ambae anaishi katika hoteli iliyo karibu na kambi hiyo ya wanajeshi wa Ethiopia katika mji wa Baidoa.
Msemaji wa waziri mkuu wa Somalia Muse Kulow amethibitisha tukio hilo na amearifu kuwa mwanajeshi mmoja amejeruhiwa katika shambulio hilo.
Hali ya usalama imeimarishwa katika eneo hilo na bara zilizo karibu na mahala palipotokea shambulio hilo zimefungwa katika mji wa Baidoa ulio kilomita 250 kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Mogadishu.
Waziri mkuu wa Somalia Ali Mohamedi Gedi na maafisa wake wako salama.
Kiongozi wa kundi la wapiganaji wenye itikadi kali Sheikh Mukhtar Robow amedai kuwa kundi lake limehusika na shambulio hilo.