BAIDOA: Viongozi wa Somalia waalikwa Saudi Arabia
24 Oktoba 2007Msemaji wa waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Somalia amesema kwamba Saudi Arabia imetoa mualiko kwa viongozi wa serikali hiyo kuhudhuria mazungumzo yakutafuta kutatua mzozo wa kisiasa unaoikumba Somalia.
Mualiko huo kwa rais Abdillahi Yusuf, waziri mkuu Ali Mohamed Gedi na spika wa bunge sheik Adan Madobe umekuja siku chache kabla ya wawakilishi wa bunge Somalia kuanza majadiliano kuhusu lini utakapomalizika muda wa miezi 30 wa waziri mkuu wa Somalia.
Msemaji wa waziri mkuu amefahamisha kuwa bwana Gedi atasafiri kuelekea Saudi Arabia leo hii kutoka mjini Addis Ababa alikokuwa anakutana na wanadiplomasia wa Umoja wa Afrika na wale wa Ethiopia.
Haijajulikana bado iwapo rais Yusuf au spika wa bunge wameukubali mualiko huo.
Rais wa mpito wa Somalia na waziri wake mkuu waliingia madarakani kwa kuungwa mkono na Ethiopia mwaka 2004 baada ya kufanyika mazungumzo ya amani nchini Kenya lakini kuanzia mapema mwaka huu viongozi hao wamekuwa hawaelewani hasa kutokana na kuwa na mawazo tafauti juu ya kushughulikia mapato baada ya kugundulika kuwa kuna uwezekano wa Somalia kuwa na nishati ya mafuta.