1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAIDOA: Ethiopia yapeleka vifaru kusini mwa Somalia

22 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCh7

Serikali ya Ethiopia imepeleka vifaru na vifaa vingeni katika uwanja wa vita siku ya tatu ya mapigano makali kati ya wanajeshi wa Somalia na wanamgambo wa mahakama za kiislamu kusini mwa Somalia.

Wapiganaji wa kiislamu wameapa kupigana vita vya jihad dhidi ya Ethiopia. Kamanda wao, Hassan Bullow, amesema watapambana na adui wanaoivamia nchi yao.

Waziri wa habari wa serikali ya mpito ya Somalia, Ali Juma, amesema mapigano bado yanaendelea baina ya pande hizo mbili, machafuko mengi yakiripotiwa katika vitongoji vya Baidoa vya Idale na Dinsoor.

Mapigano hayo yamezitatiza juhudi za mjumbe maalumu wa Umoja wa Ulaya, Louis Michel, aliyekuwa amefaulu kuzishawishi pande hizo mbili kurejea katika mazungumzo ya kutafuta amani.

Akizungumza kuhusu mapigano hayo nchini Somalia, Michel amesema machafuko hayatautanzua mgogoro huo. Amesisitiza kwamba njia ya pekee ya kuondokana na mzozo huo ni kuyaanzisha tena mazungumzo ya Khartoum ya kutafuta amani.