BAGHDAD Mateka wa Ufilipino aachiliwa huru nchini Irak
22 Juni 2005Mateka mmoja wa rehani raia wa Ufilipino ameachiliwa huru nchini Irak, baada ya kuzuiliwa kwa kipindi cha miezi minane. Roberto Tarongoy, alitekwa nyara tarehe mosi mwezi Novemba mwaka jana, pamoja na wafanyakazi wengine, wakati wanamgambo walipoyavamia makazi ya tajiri wao mjini Baghdad.
Wafanyakazi wanne waliachiliwa, lakini inaaminiwa kundi la watekaji nyara bado linamzuilia Roy Hallums, raia wa Marekani.
Rais wa Ufilipino, Gloria Arroyo, amesema Tarongoy yumo mikononi mwa wanadiplomasia wa Ufilipino, na atasafiri kurudi nyumbani wakati wowote.
Rais Arroyo aliwaondoa wanajeshi wa Ufilipino kutoka Irak mwezi Julai mwaka jana, baada mfilipino mwengine kutekwa nyara nchini humo. Mateka huyo aliachiliwa baada ya hatua hiyo, lakini rais Arroyo alikosolewa na Marekani na washiriki wengine.