Baghdad. Iraq yanyakua kombe.
30 Julai 2007Wairaq wanasherehekea ushindi wa nchi yao katika kombe la mataifa ya Asia katika soka, dhidi ya timu iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya ushindi Saudi Arabia.
Timu ya taifa ya Iraq imeishinda Saudi Arabia kwa bao 1-0 nchini Indonesia.
Bao hilo lilipatikana katika dakika ya 72 baada ya nahodha wa Iraq Younis Mahmoud kuuweka mpira wavuni kwa kichwa.
Risasi zilifyatuliwa hewani katika shamra shamra hizo katika mji mkuu Baghdad, licha ya marufuku iliyowekwa na serikali dhidi ya kufyatua risasi.
Polisi katika mji huo mkuu na mji wa Kut wameripoti kuwa kiasi cha watu saba wameuwawa na zaidi ya watu 50 wamejeruhiwa kutokana na risasi zilizokuwa zikifyatuliwa hovyo.
Bomu lililokuwa katika gari liliteguliwa na mtu mmoja anayetuhumiwa kuwa ni mpiganaji alikamatwa katika wilaya ya mjini Baghdad.
Maafisa wameanzisha utaratibu wa kuzuwia magari kutembea usiku kufuatia shambulio la kujitoa muhanga katika gari dhidi ya watu waliokuwa wakishangilia baada ya ushindi wa Iraq katika mchezo wa nusu fainali , shambulio ambalo limeuwa watu kadha siku chache zilizopita.