Bado wiki mbili kabla ya ligi ya Uingereza kunguruma
2 Agosti 2010Tuanze na soka.
Ikiwa zimesalia wiki mbili hadi kuanza kwa msimu mpya wa soka katika premier League nchini Uingereza, mabingwa Chelsea na Manchester United ambazo ni timu zinazoonekana kuwania ubingwa wa msimu huu zinajitayarisha kwa dhidi ya upinzani mkubwa kutoka kwa Manchester City ambayo imetumia fedha nyingi kuwapata mastaa kadha.
Wakati kocha wa Chelsea Carlo Ancelotti na bosi wa Manchster United Sir Alex Ferguson wameridhika na kufanya mabadiliko madogo katika vikosi vyao, meneja wa Manchester City Roberto Mancini amekuwa akiwakaribisha mastaa wapya.
Mancini ametumia kitita cha pauni milioni 80 kwa wachezaji wanne, Yahya Toure kutoka Barcelona, mchezaji wa pembeni David Silva kutoka Valencia, Alexander Kolarov kutoka Lazio Rome na mlinzi Jerome Boateng kutoka Hamburg SV.
Matumizi ya fedha nyingi hayaonekani kuishia hapo kwani Mancini anatamani kuwapata Mario Baloteli kutoka mabingwa wa kombe la champions league Inter Milan na pia anatafuta saini ya James Milner wa Aston Villa.
Huko nchini Ufaransa msimu unaanza rasmi Jumamosi ijayo huku wachezaji pamoja na mashabiki wakitambua wazi kuwa kuna haja ya mabadiliko makubwa kuweza kuiweka vizuri hadhi ya soka la nchi hiyo baada ya kampeni iliyoleta maafa ya kombe la dunia nchini Afrika kusini.
Timu ya taifa ilikumbana na wakati mgumu uwanjani , ikipoteza michezo miwili kati ya mitatu katika kundi lake na kutoka sare mmoja.
Wachezaji wanajiweka tayari kwa ghadhabu ya mashabiki wa nchi hiyo kutokana na vituko vilivyoonyeshwa na timu hiyo huko Afrika kusini ikiwa ni pamoja na mgomo wa siku moja kufanya mazowezi.
Kocha wa Liverpool ya Uingereza Roy Hodgson amekiri jana Jumapili kuwa ana wasi wasi na kuwapo tayari kwa timu yake wakati wa kuanza Premier League.
Hodgson aliweza kumuingiza kikosini Joe Cole aliyetia saini kuichezea timu hiyo majira haya ya joto, pamoja na mchezaji mwenzake katika timu ya taifa Steven Gerrard, Jamie Carragher na Glen Johnson kwa mara ya kwanza jana Jumapili wakati timu hiyo ilipolala kwa bao 1-0 dhidi ya Borussia Moenchengladbach katika mchezo wa kirafiki. Lakini kocha huyo amesema kuwa ilikuwa vigumu sana kujitayarisha kwa ajili ya msimu mpya kutokana na wachezaji wake wazoefu kutokuwapo kambini.
Kocha wa Chelsea Carlo Ancelotti amesisitiza leo kuwa klabu yake haitamuuza kamwe mlinzi wa pembeni kushoto Ashley Cole, ambaye anahusishwa na kwenda katika timu ya Real Madrid, ambayo hivi sasa inafunzwa na kocha wa zamani wa Chelsea Jose Mourinho. Ripoti zinasema kuwa Mourinho, ambaye alikuwa karibu sana na Cole wakati akiifunza timu hiyo ya Uingereza ya Stamford Bridge, yuko tayari kutumia fedha nyingi kumpata mlinzi huyo.
Naye meneja wa Everton David Moyes amekiri jana Jumapili kuwa nyota wa timu ya taifa ya Marekani Landon Donovan huenda akawa ghali sana kwa timu yake kuweza kumpata tena kwa mkopo kuja kuchezea timu hiyo ya Goodison Park.
Donovan alikaa kwa muda wa miezi mitatu na klabu hiyo ya premier League mwanzoni mwa mwaka huu na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 amedokeza kuwa atakubali kurejea.
Carles Puyol ametangaza jana Jumapili kuwa ataendelea kuichezea timu ya taifa ya Hispania kwa muda wa miaka miwili zaidi, hadi fainali za kombe la mataifa ya Ulaya zitakazofanyika mwaka 2012. Puyol mwenye umri wa miaka 32 alidokeza baada ya ushindi wa Hispania katika kombe la dunia Julai mwaka huu kuwa huenda akajiuzulu kutoka timu ya taifa.
Nicolas Anelka aliingia uwanjani kwa mara ya kwanza jana tangu pale alipofungishwa virago kutoka katika timu ya taifa ya Ufaransa huko Afrika kusini lakini alishindwa kuzuwia kipigo cha bao 2-1 dhidi ya Eintracht Frankfurt jana katika mchezo wa kifariki mjini Frankfurt.
Na huko katika bara la Afrika vigogo wa soka barani Afrika Enyimba ya Nigeria imeshindwa kutoroka mara hii baada ya kubanwa na Zanaco ya Zambia na kutolewa katika kinyang'anyiro cha kuwania ubingwa wa bara la Afrika. Ikihitaji magoli manne bila majibu katika ngome yao ya mjini Aba ili kulazimisha mikwaju ya penalti dhidi ya mabingwa hao wa Zambia Zanaco, Enyimba ilimudu tu ushindi wa mabao 2-0. Mabingwa hao wa Zambia wamesonga mbele kwa jumla ya mabao 4-2.
Lakini SuperSport ya Afrika kusini imeendelea kudorora wakati ilipoteleza kwa bao 1-0 dhidi ya FUS Rabat ya Morocco. Sfaxien imefanikiwa nayo kusonga mbele kwa mabao 3-1 dhidi ya Petro Atletico ya Angola, na Al Hilal ya Sudan nayo ilifanikiwa kuingia katika ligi hiyo ya mabingwa ngazi ya ligi ndogo baada ya kuishinda CAPS ya Zimbabwe kwa mabao 3-1 mjini Harare.
Nayo Al Ahly ya Misr ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ismailia pia ya Misr katika pambano lililofanyika mjini Cairo, wakati JS Kayblie ya Algeria inaongoza kundi lao baada ya kuishinda Heartland ya Nigeria kwa bao 1-0 katika mji wa Tizi-Ouzou hapo kabla.
Argentina haijamtafuta mrithi wa kiti cha ukocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo kufuatia kuondoka kwa Diego Armando Maradona, amesema meneja Carlos Bilardo jana.
Julio Grondona rais wa shirikisho la kandanda nchini Argentina hajazungumza na mtu yoyote na hajaniambia kitu chochote, amesema Bilardo. Tunasubiri. Kitu chochote kinaweza kutokea.
Na Mdachi Han Berger anatarajiwa kuchukua hatamu za kuifunza Australia kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa nchi hiyo mwezi huu dhidi ya Slovenia, limesema shirikisho la kandanda la Australia leo.
Mkurugenzi wa ufundi wa kikosi hicho cha soccerroos amepandishwa cheo na kujukua wadhifa wa meneja wa mpito wakati shirikisho hilo linaangalia njia ya kumteua mtu mwingine kuchukua nafasi ya kocha wa zamani Pim Verbeek , ambaye ameondoka baada ya fainali za kombe la dunia mwaka huu huko Afrika kusini.
FIFA imewapatia maafisa wa chama cha kandanda nchini Iraq mwaka mmoja zaidi kuwapo madarakani wakijitayarisha kwa uchaguzi wa chama hicho, baada ya mizozo wa kimadhehebu na kusababisha shirikisho hilo kushindwa kufanya uchaguzi kwa ajili ya viongozi wapya.
Uamuzi wa FIFA uliotolewa leo una maana unaondoka kitisho cha Iraq kuondolewa uanachama kutoka katika shirikisho hilo la kandanda duniani na kuiruhusu timu ya taifa kujitayarisha kutetea ubingwa wake wa bara la Asia Januari mwakani.
Na sasa ni riadha:
Christophe Lemaitre amekuwa mtu wa kwanza kuwa bingwa wa michezo mitatu ya ubingwa wa riadha barani Ulaya akishinda mbio za mita 100, 200 na 100 kupkezana vijiti lakini juhudi zake hazikutosha kuiweka Ufaransa juu ya Urusi katika oridha ya medali jana.
Urusi ilimaliza mashindano hayo ikiwa ya kwanza kwa kunyakua medali 10 za dhahabu, mbili zaidi ya Ufaransa , ambayo imepata medali 8 na Uingereza ikiwa ya tatu kwa kupata medali 6 za dhahabu.
Ujerumani imechukua nafasi ya 4 ikiwa na medali 4 za dhahabu, sita za fedha na 6 za shaba.
Na hadi kufikia hapo ndio sina budi kusema tunaufunga ukurasa wetu huu wa michezo mwishoni mwa juma. Mimi ni Sekione Kitojo hadi mara nyingine kwaherini.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre/afpe/dpae
Mhariri:Josephat Charo