Bado siku nne uchaguzi Ujerumani
19 Septemba 2013Na pia chama kipya cha AfD kinachopinga muungano wa Ulaya kinaelekea kupata uwezekano wa kuingia katika bunge la Ujerumani kwa mara ya kwanza. Taarifa zaidi na Sekione Kitojo.
Uchunguzi uliofanywa na shirika la habari la DPA katika zaidi ya miji 20 mikubwa ya Ujerumani , umegundua kuwa maafisa wa uchaguzi wanaripoti ongezeko kubwa la kura zilizopigwa kwa njia ya posta, ikilinganishwa na mwaka 2009, wakati asilimia 21.4 ya wale waliopiga kura zao walipata karatasi za kura kabla na kuzirejesha kwa njia ya posta.
Kura yoyote ambayo haitarejeshwa katika ofisi ya tume ya uchaguzi ifikapo saa 12 jioni kwa saa za Ulaya ya kati siku ya Jumapili haitahesabiwa. Maafisa wa shirikisho wanashauri kwamba kura hizo zitumwe kwa njia ya posta leo Alhamis(19.09.2013) ili kuhakikisha kuwa zinafika katika wakati muafaka.
Kura kupitia posta
Ujerumani inaruhusu upigaji wa kura kupitia posta kutokea nyumbani ama wakati mtu yuko safarini , kama njia mbadala ya kujipanga mstari katika vituo vya kupigia kura siku ya Jumapili. Kiasi ya wapigakura milioni 9.4 walitumia njia hiyo ya posta mwaka 2009. Ujerumani ina wapiga kura milioni 61.8 waliojiandikisha kupiga kura mwaka huu.
Wakati huo huo chama kipya kinachopinga muungano wa Ulaya kiko ukingoni mwa kuingia katika bunge la Ujerumani kwa mara ya kwanza , umeonesha uchunguzi wa maoni ya wapiga kura , na kuweka kiwingu kwa juhudi za kansela Angela Merkel kuendeleza muungano wake wa siasa za wastani za mrengo wa kulia na kukwaza sera zake za eneo la sarafu ya euro.
Merkel ana hakika
Merkel bado ana hakika ya kupata kipindi cha tatu cha uongozi katika uchaguzi wa hapo Jumapili. Lakini chama chagua mbadala kwa Ujerumani AfD, ambacho kinanyanyuliwa kutokana na wimbi upinzani kuhusu msaada wa uokozi kwa mataifa yenye madeni ya upande wa kusini mwa Ulaya , kinaweza kuligawa zaidi bunge la Ujerumani , na kumlazimisha Merkel kuunda muungano wa serikali na mahasimu wake wa Social Democratic , SPD , katika kile kinachoelezwa kuwa muungano mkuu wa siasa za mrengo wa kulia na kushoto.
Kukubalika kwa chama hicho , ambacho kinapendelea kuyaondoa mataifa dhaifu kutoka uanachama wa sarafu ya euro , utaleta hali ya hofu miongoni mwa mataifa ya Ulaya na hali hiyo inaweza kuzusha wasi wasi pia katika masoko ya fedha, licha ya kuwa sauti yake katika bunge bado itakuwa ndogo.
Lakini wanachama wa chama cha kansela Angela Merkel wamebadilisha mbinu sasa siku nne kabla ya uchaguzi na wanakishambulia chama hicho.
Chama cha kansela Angela Merkel cha Christian Democratic ambacho kilikidharau chama hicho kidogo cha AfD katika kampeni hadi sasa, kimemuweka mtu wao maarufu kabisa , waziri wa fedha Wolfgang Schauble kukishughulikia chama hicho kipya.
"Watu hawa wanadai kuwa tutakuwa katika hali bora zaidi ikiwa tutaachana na sarafu ya euro", waziri huyo mwenye umri wa miaka 71 ameliambia gazeti la Die Welt. Madai hayo si ya kweli kabisa, hayana ukweli na ni hatari sana kwa ustawi wetu. amemaliza Schauble.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / dpae
Mhariri: Josephat Charo