Bado kuna malalamiko mengi ya kucheleweshwa haki Tanzania
2 Februari 2022Rais Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo wakati wa kilele cha wiki ya sheria nchini Tanzania kilichofanyika hii leo jijini Dodoma.
Amesema kuwa licha ya kuwepo na changamoto kadha wa kadha katika utendaji kazi ya utoaji haki katika mahakama nchini Tanzania, kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi ya kucheleweshewa haki na wakati mwingine kunyimwa kabisa haki zao katika vyombo vya sheria ikiwemo mahakama.
Wanawake wagandamizwa zaidi ?
Amesema malalamiko mengi ya wananchi yapo kwenye masuala ya mirathi huku wanawake wakionekana kukandamizwa zaidi.
Rais Samia ameongeza kusema kuwa mahakama inapaswa kuzingatia sheria ili kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi.
Kadhalika Rais Samia amezitaka wizara za mawasiliano na teknolojia, Elimu na vyuo vikuu vyote nchini Tanzania kuhakikisha wanafunzi wote wanapatiwa ujuzi mpya ambao ni tofauti na wahitimu wa miaka ya nyuma iliyopita ili kwendana na matakwa ya mabadiliko ya teknolojia katika suala zima la utoaji haki.
Changamoto za kiafya
Awali Jaji mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma alisema kuwa uwepo wa mifumo ya mikutano kwa njia ya video imesaidia mahakama nchini Tanzania kuendesha kesi hasa wakati huu wa janga la Corona na hivyo mabadiliko ya teknolojia yamesaidia katika utoaji haki.
Sherehe za kilele cha wiki ya sheria nchini Tanzania zimefanyika leo Jumatano jijini Dodoma huku kukiwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi ya kucheleweshewa haki na wakati mwingine kunyimwa kabisa haki zao katika vyombo vya sheria ikiwemo mahakama huku wanawake wajane wakionekana kuwa wahanga wakubwa katika masuala mazima ya kesi za mirathi.