Baba Mtakatifu amaliza ziara yake Brazil
14 Mei 2007Wakati Baba Mtakatifu Benedikt, au “Papa Bento” kama Wabrazil wanavyomuita, alipopanda ndege mjini Sao Paolo, aliaga nchi ambayo raia wake walimshangilia kwa muda wote wa ziara yake ya siku tano. Watu milioni mbili waliweza kumuona Papa kwa macho yao. Katika misa ya mwisho mjini Aparecida, waumini walifanya shangwe kama kwenye uwanja wa mpira.
Lakini ilionekana pia kwamba matarajio fulani hayakufikiwa. Waumini waliofika kwenye misa ya Aparecida hawakuzidi idadi ya laki tano. Kabla ya hapo watu millioni moja walitarajiwa kutembelea misa hiyo. Kwa hiyo, licha ya shangwe hiyo yote, yaliyowekwa wazi pia ni kwamba kanisa katoliki linakabiliwa na hali ngumu Amerika Kusini. Kila mwaka mamia ya Wakatoliki wanatoka kanisa lao na kuelekea madhehebu mengine. Katika juhudi zake za kupambana na changamoto hiyo, Baba Mtakatifu alidai kanisa katoliki la Amerika Kusini litafute njia mpya. Sura ya kikatoliki ya Amerika Kusini iko hatarini, Benedikt alisema.
Bila ya kutaja nchi kama Venezuela, Papa huyu alikosoa vikali sera fulani zilizopo katika nchi hizo: “Kuna maendeleo mazuri ya kidemokrasia, lakini pia kuna aina ya mamlaka makali na nadhari fulani zilizosemekana kutofaa tena na ambazo hazikubaliani na mawazo ya kikristo juu ya binadamu na jamii.”
Vita dhidi ya umaskini ndio msingi wa kanisa lake, alisema Papa Benedikt wa 16 katika hotuba yake mbele ya mkutano wa maaskofu wa Amerika Kusini. Dini ya kikristo haimaanishi tu maadili ya maisha ya kibinafsi, bali pia katika maadili ya kijamii na ya kisiasa. Wakati huo huo lakini, Papa alionya kanisa lisijiingize katika siasa: “Ikiwa kanisa litajihusisha kama chombo cha kisiasa, basi haliwezi kuwasaidia zaidi maskini na kuleta usawa, bali ni kinyume chake. Kwa sababu litapoteza uhuru wake na mamlaka yake ya maadili.”
Msingi wa kupambana na umaskini na njaa na kuleta jamii yenye usawa ndio kumuamini Mungu na kuishi maisha ya kikristo, alisisitiza Baba Mtakatifu. Si nadhari ya Kikomunisti wala mfumo wa ubepari uliweza kuondosha umaskini.
Kwenye ziara yake ya kwanza kwenda Amerika Kusini tangu kuingia katika cheo chake miaka miwili iliyopita, Benedikt wa 16 aliwaonya waumini kutokubali utoaji mimba au uzazi wa mpango. Vile vile alirudia mwito wake kwa Wabrazil kuheshimu ndoa na familia.