1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baba mtakatifu aizuru Uingereza

16 Septemba 2010

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba mtakatifu Benedict wa 16, amewasili nchini Uingereza kuanza ziara yake ya kihistoria ya siku nne ambako anakutana na Malkia Elizabeth ll wa Uingereza

https://p.dw.com/p/PDc6
Baba mtakatifu Benedict XVI kulia akiwa na mume wa malkia alipowasili Edinburgh ScotlandPicha: AP

Baba mtakatifu amewasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Edinburgh, Scotland, ikiwa ni safari yake ya 17 tokea alipochaguliwa kushika wadhifa huo mwaka 2005. Pia hiyo ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa kanisa katoliki duniani kutembelea Uingereza tokea Papa John Paul wa pili alipoizuru mwaka 1982.

Mamia ya watu wamejitokeza kumlaki kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki ambalo katika siku za hivi karibuni limegubikwa na kashfa ya ngono dhidi ya watoto, vitendo ambavyo vilifanywa na makasisi wa kanisa hilo.

Ndege iliyombeba Baba mtakatifu iligusa ardhi ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Edinburg milango ya saa nne na dakika 15 saa hapa Ujerumani huku ulinzi ukiwa wa hali juu ya kabisa. Amepokewa na mume wa Malkia, Prince Philip.

Baba mtakatifu amepangiwa kuendesha misa ya wazi. Waandalizi wa misa hiyo wameweka kiingilio cha Euro 30 kwa kila atakayeingia kwenye misa hiyo, hatua ambayo imelaumiwa

Kabla ya kuanza safari hiyo, mmoja wa wasaidizi waandamizi wa Baba mtakatifu, Kadinali Walter Kasper, alitoa matamshi yaliyoiudhi Uingereza akiifananisha nchi hiyo na zile za dunia ya tatu.

Kadinali Walter alikuwa aandamane na Baba mtakatifu katika ziara hiyo, lakini kutokana na matatizo ya afya ameshindwa kufanya hivyo. Kauli yake hiyo imeshutumiwa vikali na Kanisa Katoliki la Uingereza ambalo limemtaka kuomba radhi.

Ziara hiyo inatarajiwa kukumbana na upinzani kutokana na sera za kanisa za kupinga suala la utoaji mimba pamoja na haki za mashoga.Lakini kwa wengine ni furaha kumuona Baba mtakatifu.

Baba mtakatifu anaitumia ziara hiyo kulisafisha kanisa kutokana na kashfa ya ngono dhidi ya watoto, ambapo akiwa njiani kuelekea Scotland aliwaambia waandishi wa habari anaongozana nao kuwa jukumu kubwa hivi sasa la kanisa ni kurejesha imani miongoni mwa waumini wake kufuatia kashfa hiyo.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP/TV

Mhariri:Othman Miraji