Baada ya Ugiriki na Ureno sasa ni Uhispania
29 Aprili 2010Baada ya kukutana na wakuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, Benki Kuu ya Ulaya na taasisi zingine za fedha mjini Berlin, kujadiliana njia ya kuisaidia Ugiriki inayokabiliwa na tatizo la madeni makubwa, Kansela Merkel alikariri kuwa Ujerumani itaisaidia Ugiriki lakini nchi hiyo pia inapaswa kuchua hatua zaidi.
Hata Mkuu wa IMF,Dominique Strauss-Kahn amesema, Ugiriki itapata msaada wa fedha lakini kilicho muhimu hivi sasa ni kuchukuliwa hatua za haraka. Amesema,uaminifu wa nchi za kanda inayotumia sarafu ya euro upo hatarini.
Inatathminiwa kuwa hadi mwaka 2012, IMF na nchi za kanda ya euro zitapaswa kutoa kati ya euro bilioni 120 na 135 kuisaidia Ugiriki.Ifikapo Mei 19,Ugiriki inapaswa kulipa deni la kiasi cha euro bilioni 9. Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya,Herman Van Rompuy ameitisha mkutano wa viongozi wa nchi za kanda ya Euro tarehe 10 Mei mjini Brussels.
Mgogoro wa madeni sasa umeenea katika nchi zingine za Ulaya. Kwani baada ya Ugiriki na Ureno, sasa Uhispania pia imeorodheshwa na shirika la "Standard and Poor´s" kama ni nchi isiyo na uwezo wa kulipa madeni yake. Shirika hilo hutathmini uwezo wa nchi kulipa madeni yake.
Viwango vya riba viliongezeka siku ya Jumatano, baada ya Ugiriki na Ureno hapo awali kutiwa katika orodha ya nchi zisizoaminiwa kukopeshwa. Sasa Ugiriki inalazimika kutoa riba ya asilimia 12 ili kuweza kupata mikopo mipya katika masoko ya fedha. Hiyo ni mara nne zaidi kuliko ile inayolipwa na Ujerumani.
Mhariri:P.Martin/DPA