1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Azimio kutaka kukomeshwa mzingiro wa El-Fasher lapitishwa

14 Juni 2024

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio linalotaka kukomeshwa kwa mzingiro wa kijeshi kwenye mji wa Sudan wa El-Fasher.

https://p.dw.com/p/4h15T
Ukumbi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York.
Ukumbi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York.Picha: Eduardo Munoz/REUTERS

Pendekezo hilo linataka pia kumalizwa kwa machafuko kwenye taifa hilo linaloandamwa na vita vya zaidi ya mwaka mmoja.

Wanachama 14 kati ya 15 wa Baraza la Usalama walipiga kura kuunga mkono azimio hilo lililoandaliwa na Uingereza. Urusi ilijizuia kulipigia kura azimio hilo.

Azimio hilo linazirai pande zote mbili kwa maana ya jeshi la Sudan na kundi la wanamgambo la RSF kusitisha mara moja mapigano.

Pande hizo mbili hasimu zimekuwa zikipambana kuwania udhibiti wa El-Fasher ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Darfur Kaskazini. 

Mji huo ndiyo pekee salama unaowahifadhi watu waliokimbia machafuko na mashirika ya misaada yameonya kuhusu hali mbaya ya kiutu kutokana mapambano yanayoendelea.