Azimio kukomesha udukuzi
2 Novemba 2013Rasimu ya azimio hilo ambalo nchi zote mbili za Ujerumani na Brazil imelitangaza hadharani halizitaji nchi kwa majina juu ya kwamba wanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa wamesema ni wazi kuwa lilikuwa limeikusudia Marekani ambayo imeadhirishwa kutokana na kufichuliwa kwa mpango wake mkubwa wa upelelezi wa kimataifa na mfanyakazi wa zamani wa shirika la usalama wa taifa nchini humo.
Rasimu ya azimio hilo la Ujerumani na Brazil italitaka Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lenye nchi wanachama 193 litangaze kwamba "lina wasi wasi mkubwa juu ya ukiukaji wa haki za binaadamu na dhuluma nyengine ambazo yumkini zikasababishwa kutokana na upelelezi wa aina yoyote ile wa mawasiliano ukiwemo ule wa kupindukia mipaka ya nchi."
Pia linatoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuchukuwa hatua za kukomesha ukiukaji wa haki hizo na kuweka mazingira ya kuzuwia ukiukaji wa aina hiyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba sheria za kitaifa zilizopo wajibu wake unafuatwa kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya haki za binaadamu."
Yumkini likahitaji mabadiliko
Yumkini azimio hilo likafanyiwa mabadiliko wakati litakapojadiliwa na Kamati ya tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambayo inalenga suala la haki za binaadamu. Linatazamiwa kupigiwa kura na kamati hiyo baadaye mwezi huu na badaaye kupigiwa tena kura katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi ujao.
Afisa wa balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amekaririwa akisema " Tumepokea rasimu ya azimio hilo na tutachambua maudhui yake kwa kuzingatia vigezo vyake."Wanadiplomasia kadhaa wamesema watashangaa iwapo azimio hilo halitoungwa mkono kwa kauli moja na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Brazil Dilma Rousseff wote wawili wamelaani udukuzi uliozagaa uliofanywa na Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani NSA.Madai kwamba NSA imedukiza mawasiliano ya maelfu ya simu za Wafaransa na kusikiliza simu ya mkono ya Merkel yamechemsha ghadhabu barani Ulaya.
Azimio lina uzito gani ?
Maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa kawaida utekelezaji wake unakuwa haushurutishi kisheria tofauti na maazimio yanayotolewa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye nchi wanachama 15.
Lakini maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambayo yanapata uungaji mkono mkubwa wa kimataifa yanakuwa na uzito wa kiuadilifu na kisiasa.Azimio hilo litazitaka nchi kuanzisha taratibu za usimamizi wa kitaifa zenye uwezo wa kuhakikisha kunakuwepo uwazi na uwajibikaji kwa upelelezi wa mawasiliano unaofanywa na serikali,udukuzi wao na ukusanyaji wa data za watu binafsi.
Pia litatowa wito kwa Mkuu wa masuala ya haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay kuandaa na kuchapisha ripoti kuhusu "ulindaji wa haki ya kuwa na faragha kwa zingatio la upelelezi wa ndani ya nchi na ule wa kuvuka mipaka ya nchi ikiwa ni pamoja na upelelezi wa kiwango kikubwa sana, upelelezi wa mawasiliano, udukuzi wao na ukusanyaji wa data za watu binafsi.
Mpango mkubwa sana wa upelelezi wa Marekani umefichuliwa kutokana na nyaraka zilizovujishwa kwa vyombo vya habari na mfanyakazi wa zamani wa shirika la NSA Edward Snowden.Marekani imesema haichunguzi mawasiliano ya Merkel na haitofanya hivyo kipindi cha usoni lakini haikuzungumzia iwapo iliwahi kufanya hivyo huko nyuma.
Mapema wiki hii, Umoja wa Mataifa umesema Marekani imeahidi kutoyafanyia upelelezi mawasiliano ya Umoja wa Mataifa baada ya kuripotiwa kwamba Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani NSA lilikuwa likidukiza mfumo wa mkutano wa Umoja wa Mataifa unaofanyika kwa njia ya video.
Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters
Mhariri:Caro Robi