Azerbaijan kutoa pendekezo jipya la ufadhili wa tabianchi
22 Novemba 2024Mkutano huo wa wiki mbili kwenye mji wa Baku kuna uwezekano utaingia katika muda wa ziada, huku kukiwa na maelezo muhimu kuhusu makubaliano ambayo bado hayajatolewa, achilia mbali kuafikiwa.
Soma pia: Umoja wa Mataifa wataka mataifa kuwa na utayari ili kupata makubaliano katika mkutano wa COP29
Suala kuu la kipaumbele katika mazungumzo ya COP29 mjini Baku ni kukubaliana kuhusu ufadhili mpya wa kuchukua nafasi ya ule wa dola bilioni 100 kwa mwaka ambazo mataifa Tajiri huyapa mataifa maskini ili kupunguza gesi chafuzi na kukabiliana na majanga.
Nchi zinazoendelea Pamoja na China, zinashinikiza kutolewa kiasi cha dola trilioni 1.3 ifikapo mwaka wa 2030 na zinataka karibu dola bilioni 500 ya hizo kutoka kwa mataifa yaliyostawi.
Wachangiaji wakubwa kama vile Umoja wa Ulaya wanapinga masharti ya aina hiyo, na wanasisitiza kuwa fedha za sekta binafsi lazima zijumuishwe kuelekea lengo hilo.
Azerbaijan ambayo ndio inashikilia urais wa COP29 imesema katika taarifa kuwa "imetiwa moyo na kiwango cha wepesi kinachooneshwa na washiriki” na itatoa rasimu mpya leo Ijumaa. Rasimu hiyo mpya inatarajiwa kutoa takwimu za kifedha baada ya waraka wa awali uliotolewa jana Alhamisi kusema kuwa nchi zinazoendelea zilihitaji angalau dola trilioni fulani kwa mwaka lakini ikaondoa kiasi kamili cha fedha.
Soma pia: Dunia bado imegawanyika kuhusu fedha wakati muda ukiyoyoma COP29
Ali Mohamed, mwenyekiti wa Kundi la Wajumbe wa Kiafrika, na ambaye pia ni balozi wa Kenya kuhusu tabia nchi amesema kizungumkuti ni kiasi cha fedha ambacho hakikuwekwa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ambaye aliondoka Baku baada ya kuhudhuria ufunguzi wa COP29 wiki iliyopita, alionya kuwa "kufeli sio chaguo.”
Masuala mengine yanayozusha utata – ikiwemo nani anayechangia fedha za tabianchi na vipi fedha zinachangishwa na kuwasilishwa – hayakushughulikiwa katika rasimu hiyo.
Mbali na mgawanyiko kuhusu fedha, mataifa mengi yalisema rasimu hiyo ilishindwa kuakisi udharura wowote wa kukomesha matumizi ya makaa ya mawe, mafuta na gesi -- vichochezi vikuu vya ongezeko la joto duniani.
Mkutano wa kilele wa COP28 mwaka jana Dubai, uliwezesha kufikiwa wito wa kihistoria kwa ulimwengu kuwachana na mafuta ya kisukuku.
Afisa mmoja wa Saudia akizungumza kwa niaba ya Kundi la Mataifa ya Kiarabu amesema jumuiya hiyo haitakubali rasimu yoyote ambayo inazilenga sekta zozote maalum, ikiwemo ya mafuta ya kisukuku. Nchi zilizostawi kiviwanda zinasema haiwezekani kisiasa kutoshirikisha uwekezaji wa sekta binafsi. Pia zinataka kutanuliwa kwa orodha ya wafadhili – hasa kujumuisha China, ambayo inatoa msaada wake yenyewe lakini haina wajibu wowote kwa sababu bado inaorodheshwa kama nchi inayoendelea.
Kwa sasa, fedha nyingi za mabadiliko ya tabianchi hutolewa kama mikopo, kumaanisha mataifa yanayoendelea yana madeni zaidi wakati yakiweka mipango ya kupambana na ongezeko la joto duniani.
AFP