1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ayatullah Khamenei apinga mazungumzo na Trump

22 Julai 2018

Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei, alisema mazungumzo na Rais Donald Trump "hayana maana" yoyote kwa kuwa Marekani haina tabia ya kuheshimu makubaliano wala saini zake inazoweka kwenye mikataba ya kimataifa.

https://p.dw.com/p/31sJ6
Iran  Ali Khamenei
Picha: khamenei.ir

Akizungumza kwenye mkutano na wanadiplomasia wa nchi yake siku ya Jumamosi (21 Julai), kiongozi huyo mwenye usemi wa mwisho nchini Iran, alirejelea msimamo wake kuhusu Marekani ambao alikuwa nao hata kabla ya makubaliano ya nyuklia kuwekwa saini mwaka 2015. 

"Kama nilivyosema zamani, hatuwezi kuyaamini maneno ya Marekani na hata sahihi yao, kwa hivyo mazungumzo na Marekani hayana maana," aliwaambia wanadiplomasia hao.

"Kudhani kwamba matatizo yanaweza kutatuliwa kupitia mazungumzo au mahusiano na Marekani ni kosa kubwa sana," aliongeza.

Baada ya kujiondoa kwenye makubaliano hayo muhimu ya nyuklia mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani, sasa Marekani imepania kuitenga zaidi Iran na kuongeza vikwazo kadhaa vya kiuchumi kuanzia mwezi Agosti.

Ulaya inapingana na hatua hiyo ya Marekani na imeapa kuwa itasaka njia za kuendelea na mahusiano yake ya kibiashara na Iran, ambayo kwa mujibu wa makubaliano iliacha kuendeleza mpango wake wa nyuklia ili nayo iondolewe vikwazo.

Aruhusu mazungumzo na Ulaya kuendelea

Belgien EU-CELAC Aussenministertreffen in Brüssel
Ayatullah Ali Khamenei anataka mazungumzo na Ulaya yaendelee lakini sio bila ukomo.Picha: European Union

"Mazungumzo na Ulaya lazima yaendelee, lakini nao pia hatupaswi kuwasubiria milele kuleta mapendekezo yao," alisema Khamenei.

Baada ya Marekani kujiondoa kwenye makubaliano hayo ya nyuklia, Iran iliweka wazi kwamba inataka kuendelea nayo, lakini endapo tu mataifa matano yaliyobakia yanaweza kuihakikishia kuwa haitatengwa kiuchumi kutokana na vikwazo ambavyo Marekani imeanza kuvirejesha.

Kumekuwa na wito kutoka wanasiasa wanaopendelea mageuzi ya sera nchini Iran kuitaka Iran izungumze na Marekani, mara baada ya hatua ya mwezi Mei ya Rais Trump kuiondoa nchi yake kutoka kwenye makubaliano hayo. 

Hii inatokana na hali ya kiuchumi kuzidi kuwa mbaya kwenye taifa hilo linalozalisha mafuta kwa wingi duniani. 

Rais Trump amewahi kunukuliwa akisema kuwa yuko tayari kwa makubaliano mapya ambayo siyo tu yatahusisha mitambo ya nyuklia, lakini pia mpango wa makombora wa Iran na uingiliaji wake kwenye masuala ya Mashariki ya Kati na Ghuba ambao unachukuliwa kuwa kitisho kikubwa dhidi ya mshirika mkuu wa Marekani, Israel.

Khamenei amuunga mkono Rouhani

Iranischer Präsident Hassan Rouhani
Rais Hassan Rouhani ametishia kwamba ikiwa mafuta ya Iran yatazuiwa, basi Mashariki ya Kati nzima nayo itaathirika.Picha: Getty Images/M. Gruber

Rais Hassan Rouhani mwenyewe ameshakataa maombi manane tafauti ya kukutana na Trump, kwa mujibu wa mkuu wa utumishi kwenye ofisi ya Rouhani. 

Katika hatua nyengine, Ayatullah Khamenei ameliunga mkono onyo lililotolewa awali na Rais Rouhani juu ya uzalishaji mafuta. 

Mapema mwezi Julai, Rouhani alisema kuwa endapo usafirishaji wa mafuta ghafi kutoka Iran utatishiwa, basi eneo zima la Mashariki ya Kati nalo litakuwa limetishiwa.

Rouhani hakufafanuwa undani wa onyo hilo, lakini umekuwa msimamo wa muda mrefu wa Iran kwamba itaifunga njia muhimu ya Hormuz ambayo hutumiwa na robo nzima ya meli zinazosafirisha mafuta duniani. 

"Marekani inataka hali irejee na hadhi yao iwe kama ilivyokuwa kabla ya mapinduzi ya Kiislamu ya 1979," alisema Khamenei. 

"Wanapingana na uwezo wa kinyuklia wa Iran na nguvu zake za kujitajirisha na uwepo wake kwenye eneo hili," aliongeza. Iran ilikuwa mshirika mkubwa wa Marekani kabla ya mapinduzi hayo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP/AP/Reuters
Mhariri: John Juma