Axel Witsel ajiunga na Atletico Madrid
6 Julai 2022Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 amesaini mkataba hadi Juni 30, 2023, baada ya miaka minne katika ligi kuu ya kandanda ya Ujerumani Bundesliga.
Atletico imesema katika taarifa yake kwamba Witsel sasa ni mchezaji mpya wa klabu hiyo baada ya makubaliano kuafikiwa kati ya klabu na Mbelgiji huyo. "Kiungo wetu mpya ataleta uzoefu mwingi, baada ya kucheza zaidi ya mechi rasmi 600"
Tangazo hilo linathibitisha hatua iliyochukuliwa na rais wa klabu ya Atletico Enrique Cerezo mnamo tarehe 27 mwezi Juni.
Witsel ambaye ameichezea timu ya taifa ya Ubelgiji mechi 124, anajiunga na klabu hiyo kuziba pengo lilioachwa na Hector Herrera raia wa Mexico. Atashirikiana na mchezaji mwenzake wa timu ya taifa ya Ubelgiji, Yannick Carrasco.
Baada ya kuanza taaluma yake na klabu ya Standard Liege mwaka 2006, Witsel alisonga mbele na kuichezea Benfica, Zenith Saint Petersburg na klabu ya China, Tianjin Tianhai kabla kujiunga na Borussia Dortmund mwaka 2018.
Msimu uliopita Witsel alicheza mechi 40 na kutia kimyani mabao mawili. Alishiriki pia katika timu ya taifa ya Ubelgiji katika mashindano ya kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazili na 2018 nchini Urusi na mashindano ya kombe la Ulaya 2016 na 2020.
(afpe)