1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brazil yabanduliwa nje ya Kombe la Dunia

22 Juni 2015

Australia imeibandua nje Brazil katika dimba la Kombe la Dunia la Wanawake na kujikatia tikiti ya kucheza robo fainali pamoja na Ufaransa, Ujerumani, China na wenyeji Canada

https://p.dw.com/p/1Fl4k
Frauen Fußball WM Brasilien gegen Australien
Picha: Reuters/M. Kryger

Australia iliifunga goli moja kwa sifuri timu ya Brazil ambayo ilikuwa imeshinda mechi zake zote tatu za awamu ya makundi. Wakati timu ya wanaume ikijikatia tikiti ya robo fainali katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Amerika Kusini nchini Chile, timu ya wanawake ya Brazil nayo ilifungasha virago kurudi nyumbani.

Ufaransa ilidhihirisha umahiri wake kama mojawapo ya timu zinazopigiwa upatu katika dimba hili, kwa kusajili ushindi wa tatu bila dhidi ya Korea Kusini, wakati nayo Canada ikipata ushindi wa bao moja kwa bila dhidi ya Uswisi. Cocha wa Canada John Herdman sasa huenda akacheza dhidi ya taifa la uzawa wake ikiwa England itaipiku Norway katika mpambano wa leo. Kocha wa England MARK SAMPSON amesema watajitahidi vilivyo. Mchuano mwingine wa leo ni kati ya Marekani na Colombia.

Siku ya Jumamosi, Ujerumani mabingwa wa mwaka wa 2003 na 2007 waliwagwangura Sweden mabao manne kwa moja na sasa watashuka dimbani dhidi ya Ufaransa katika mchuano wa robo fainali. Kocha wa Ujerumani Silvia Neid amesema timu yake ilistahili ushindi

Katika mchuano mwingine wa Jumamosi, China iliiwafungisha virago Cameroon kwa kuafunga goli moja kwa sifuri. Hivyo ina maana hakuna timu yoyote ya Afrika iliyotinga robo fainali.

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman