Australia yabatilisha utambuzi wa mji mkuu wa Israeli
19 Oktoba 2022Wong amesema kuwa serikali ya chama cha mrengo wa kushoto cha Labour imekubali kuutambua tena Tel Aviv kama mji mkuu. Wong ameongeza kuwa baraza la mawaziri pia limesisitiza kwamba hadhi ya Yerusalemu lazima itatuliwe kupitia mazungumzo ya amani kati ya Israeli na Wapalestina. Wong pia ameeleza kwamba Australia imejitolea katika suluhisho la pande mbili katika mzozo huo kati ya Waisraeli na Wapalestina na kwamba haitaunga mkono utaratibu utakaokiuka matarajio hayo.
Yair Lapid ashangazwa na maamuzi ya Australia
Wakati huo huo, waziri mkuu wa Israel Yair Lapid, ameelezea kushangazwa na kubadilika kwa msimamo huo wa Australia. Katika taarifa, Lapid amesema kuwa Yerusalemu ni mji mkuu wa milele wa Israeli usiogawanyika na hakuna chochote kitakachobadilisha hilo.
Wong amesema kuwa idara yake ilifanya makosa kwa kusasisha tovuti yake kuhusu sera ya Australia iliyobadilishwa kuhusu mji mkuu wa Israel kabla ya baraza la mawaziri kuthibitisha mabadiliko hayo na kuongeza kwamba hali hiyo ilisababisha ripoti zinazokinzana za vyombo vya habari kuhusu msimamo wa Australia kabla ya tangazo la Wong.
Lapid alionekana kulaumu mkanganyiko huu wa vyombo vya habari kwa Australia kubadilisha sera yake. Lapid ameongeza kuwa kwa kuzingatia jinsi uamuzi ulivyofanywa nchini Australia, kama majibu ya haraka kwa ripoti ya makosa katika vyombo vya habari, mtu anaweza tu kutumaini kuwa katika masuala mengine, serikali ya Australia itakuwa makini zaidi. Wizara ya mambo ya nje ya Israel, imesema itamuita balozi wa Australia kuelezea kufadhaishwa na uamuzi huo kwa kuzingatia mawazo mafupi ya kisiasa.
Palestina yapongeza uamuzi wa Australia
Afisa wa ngazi ya juu wa mamlaka ya Palestina Hussein Al-Sheikh amepongeza uamuzi huo wa Australia na uthibitisho wake kwamba mustakabali wa uhuru wa Yerusalemu unategemea suluhisho la kudumu kulingana na uhalali wa kimataifa.
Mnamo mwezi Desemba mwaka 2018, Waziri mkuu wa zamani wa kihafidhina Scott Morrison aliutambua rasmi Yerusalemu Magharibi kama mji mkuu wa Israel ijapokuwa ubalozi wa Australia ulibakia mjini Tel Aviv. Wong aliitaja hatua ya Morrison kuwa isiyofaa kimataifa and mchezo aliouita kuwa wa kijinga ili kushinda uchaguzi mdogo katika eneo la Sydney lenye idadi kubwa ya Wayahudi. Morrison, ambaye bado ni mbunge wa upinzani, amesema uamuzi huo wa serikali ulikuwa wa kukatisha tamaa.
Lakini kiongozi wa upinzani Peter Dutton aliuacha mlango wazi kwa wahafidhina kuachana na sera za Waziri mkuu wa zamani bwana Scott Morrison. Dutton amewaambia wanahabari kwamba watatoa tangazo kuhusu sera yao wakati wa maandalizi ya uchaguzi ujao. Uchaguzi huo unatarajiwa mnamo mwaka 2025.