Australia yaamuru watu kuondoka maeneo yaliokumbwa na moto
2 Januari 2020Moto huo ulilikumba eneo la kusini mashariki mwa Australia katika mkesha wa mwaka mpya na kusababisha vifo vya watu wapatao wanane na kuteketeza zaidi ya nyumba 1,300.
Waziri Mkuu wa jimbo la New South Wales, Gladys Berejiklian ametangaza hali ya hatari kwa muda wa siku saba ambayo itaruhusu kuwaondoa kwa lazima watu kuanzia kesho Ijumaa. Berejiklian amesema hawauchukulii kwa mzaha uamuzi huo, lakini pia wanataka kuhakikisha wanachukua kila tahadhari kujiandaa kwa kile ambacho kinaweza kuwa kibaya zaidi siku ya Jumamosi.
Wakaazi na watalii katika maeneo ya ndani ndani ambayo yanajumuisha pia hoteli za kifahari kwenye milima ya theluji, wameamriwa kuondoka, huku watu wakipewa muda wa saa 24 kufanya hivyo kabla joto halijasababisha upepo mkali na viwango vya joto kuwa juu ya nyuzi joto 40 za Celsius.
Hali ya hewa itasababisha mazingira ambayo maafisa wanasema yatakuwa mabaya zaidi siku ya Jumamosi kuliko siku ya Jumanne, na hivyo kuwa siku mbaya zaidi tangu kuzuka kwa janga la moto kwenye msitu kwa miezi kadhaa.
Idadi ya waliokufa inahofiwa kuongezeka
Hadi sasa watu wapatao 18 wamekufa tangu kuzuka kwa majanga ya moto Australia na kuwa wasiwasi kwamba idadi hiyo inaweza ikaongezeka, huku maafisa katika jimbo la Victoria wakisema kuwa watu 17 hawajulikani walipo.
Kwa muda wa siku mbili watalii wengi na wakaazi waliishi bila ya umeme wala mawasiliano, kabla ya maafisa leo kutangaza kuwa baadhi ya barabara ni salama na hivyo zinaweza kutumika tena.
Waziri wa Usafriti wa New South Wales, Andrew Constance amesema zoezi la kuwaondoa watu ni kubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa katika eneo hilo, huku kukiwa na foleni ndefu ya magari katika barabara inayoelekea Sydney na Canberra kutokana na maelfu ya watu kukimbia.
Meli mbili za jeshi la wanamaji zimewasili Mallacoota ambako watu walijazana katika maeneo ya pwani kwa saa kadhaa katika mkesha wa Mwaka Mpya wakati ambapo moto ulizuka kwenye mji mmoja ulioko ndani ndani, kuanza kuwahamisha hadi watu 4,000 katika operesheni ambayo maafisa wanasema inaweza ikachukua wiki kadhaa.
Janga hilo limechochea maandamano ya kuitaka serikali kuchukua haraka hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo wanasayansi wanasema yanasababisha kuongezeka na kuwepo kwa moto wa misituni kuwaka kwa muda mrefu. Waziri Mkuu wa Australia, Scott Morrison amesema leo kuwa juhudi zinafanywa kuhakikisha wanazisaidia jamii zilizoathiriwa.
Vyanzo: AFP, DPA