AU yaitaka EU kuondoa vikwazo dhidi ya Shadary
27 Novemba 2018Baraza la Usalama na amani la Umoja wa Afrika limeutaka Umoja wa Ulaya kuondoa vikwazo dhidi ya chaguo la mrithi wa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Joseph Kabila chini ya mwezi mmoja kabla ya uchaguzi wa kihistoria nchini humo.
Mgombea wa chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary ambaye ni waziri wa zamani wa ndani, aliwekewa vikwazo na Umoja wa ulaya mwaka jana kwa kuzuwia hatua za uchaguzi pamoja na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu.
Taarifa ya pamoja ya Umoja wa Afrika, bila ya kumtaja Shadary, imesema kuondolewa kwa vikwazo kutasaidia kuelekea katika uchaguzi huru, wa haki, unaoaminika na wa amani nchini Congo.
Taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini la Afrika ya kati hapo Desemba 23 linakabiliwa na kile ambacho huenda ni mabadiliko ya kwanza ya madaraka kwa amani, na demokrasia.
Wapinzani wanahofu kwamba Kabila, ambaye ameitawala nchi hiyo tangu mwaka 2001, ataendelea na madaraka nyuma ya pazia iwapo Shadary atashinda.