AU kujadili unachama wa Mali, Burkina Faso na Guinea
17 Februari 2023Faki ameliambia shirika la habari la AFP kwamba suala hilo bado halijadiliwa lakini kutakuwa na mkutano wa baraza la amani na usalama ambao utaangazia maombi hayo bila ya kutoa muda maalumu.
Mataifa hayo matatu kutoshiriki mkutano wa kilele
Uanachama wa mataifa hayo matatu umesimamishwa kutoka kwa Umoja huo wa Afrika na Jumuiya ya Kiuchumi ya Kikanda ya mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS), baada ya kupitia mapinduzi ya kijeshi tangu 2020, na hayawezi kushiriki katika mkutano wa kilele wa mwishoni mwa wiki hii katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.
Wanadiplomasia waanza kushinikiza kujumuishwa kwa mataifa hayo
Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo za Afrika Magharibi walianza kushinikiza kujumuishwa tena kwa mataifa yao katika Umoja huo wa mataifa wanachama 55. Siku ya Alhamisi (16.02.2023) walikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro, Dhoihir Dhoulkamal, ambaye nchi yake itashikilia urais wa kupokezana wa Umoja wa Afrika.
Mawaziri hao watatu walikuwa wametangaza kampeni yao ya pamoja ya kidiplomasia wiki iliyopita katika mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou. Waziri wa Mambo ya nje wa Mali, Abdoulaye Diop, pia alifanya mikutano na Rais Sahle-Work Zewde wa Ethiopia na wenzake wa Rwanda na Algeria.
Mashauriano kuendelezwa
Wizara ya mambo ya nje ya Mali imesema ujumbe huo wa pamoja utaendelea na mashauriano na Faki, rais wa visiwa vya Comoro Azali Assoumani, afisa mmoja mkuu wa ECOWAS na mawaziri wengine wa mambo ya nje. Wizara hiyo imeendelea kusema kuwa kusimamishwa uanachama wa mataifa hayo matatu, kunazuia uungwaji mkono wa kikanda na kimataifa katika kipindi cha mpito kuelekea utawala wa kiraia unaoendelea katika mataifa hayo matatu ya eneo la Sahel.
Mkutano kuharakisha eneo la biashara huria
Mkutano wa kilele wa siku mbili wa Umoja wa Afrika unaoanza kesho Jumamosi, unalenga kuharakisha utekelezwaji wa eneo la biashara huria katika bara hilo. Makubaliano ya biashara huria katika bara Afrika, AfCFTA, yanayotambuliwa kama mkataba mkubwa zaidi wa biashara huria duniani kwa misingi ya idadi ya watu, yanalenga kukuza biashara ya ndani ya Afrika kwa asilimia 60 ifikapo mwaka 2034 kwa kuondoa karibu ushuru wote.