Mkutano wa kilele wa AU waanza Afrika Kusini
14 Juni 2015Masuala mengine ambayo yanatarajiwa kupewa kipaumbele katika mkutano huo ni kitisho cha makundi yenye itikadi kali ya kiislamu, kama Boko Haram ambayo inaihangaisha Nigeria, mojawapo ya nchi muhimu katika Umoja wa Afrika.
Mtafiti katika Taasisi ya Afrika Kusini kuhusu Uhusiano wa Kimataifa, Tjiurimo Hengari, anasema miaka miwili ijayo itakuwa yenye changamoto kubwa kwa Umoja wa Afrika, hususan kutokana na wimbi la baadhi ya viongozi wa nchi za bara hilo kutaka kubadilisha katiba za nchi zao ili waweze kugombea muhula wa tatu au wa nne.
Hatua ya rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kuamua kugombea muhula wa tatu, ambao wapinzani wanasema inakwenda kinyume na katiba, imeitumbukiza nchi hiyo katika mzozo ambao tayari umewauwa watu 40 na kusababisha wengine takribani 100,000 kuikimbia nchi hiyo.
Masuala yenye utata
Hata hivyo, mkutano huo wa kilele ambao aghalabu huyakwepa masuala yenye utata, unaweza kughubikwa na sakata la rais wa Sudan Omar al-Bashir ambaye amewekewa waranti wa kukamatwa wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu,ICC anayetarajiwa kuwasili nchini humo. Rais huyo anatuhumiwa kutenda uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, na Afrika Kusini kama mwanachama wa mkataba wa Roma ulioiunda ICC, inao wajibu wa kumkamata.
Msemaji wa Umoja wa Afrika, AU, Molalet Tsedeke, amelithibitishia shirika la habari la AFP kuwa rais al-Bashir anatazamiwa kuhudhuria mkutano huo.
Marais wa kiafrika wamegawika kuhusu mkataba ulioianzisha mahakama ya ICC, na mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Januari mwaka huu aliwataka wenzake kuziondoa nchi zao katika mkataba huo.
Mugabe kung'ara jukwaani
Miongoni mwa viongozi watakaopanda jukwaa la mkutano huo leo Jumapili ni mwenyekiti wa AU rais Robert Mugabe,na mwenyeji, rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma. Rais mpya wa Nigeria Muhammadu Buhari vile vile anatarajiwa kushiriki katika mkutano, lakini marais wa nchi nyingine zenye uchumi mkubwa barani Afrika, Edouardo dos Santos wa Angola, na Abdel Fatah al-Sisi wa Misri hawatashiriki.
Mkutano huu wa kilele unafanyika nchini Afrika Kusini miezi miwili tu baada ya kuzuka kwa ghasia za chuki dhidi ya wageni, ambazo ziliwalenga wahamiaji kutoka nchi za kiafrika. Ghasia hizo zilizichukiza nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika, ambazo raia wake waliathiriwa zaidi. Raia saba wa nchi za kiafrika waliuawa katika ghasia hizo zilizoanzia katika mji wa Mashariki wa Durban.
Katika kile ambacho mchambuzi wa sera za Umoja wa Afrika Liesl Louw- Voudran nachokiita ''mwenendo usio wa kawaida'', suala la chuki ya wageni litajadiliwa katika kikao cha faragha, kabla ya ufunguzi rasmi wa mkutano leo hii.
Aidha, mkutano huo utalizungumzia tatizo la wahamiaji wa kiafrika na kutoka nchi za Mashariki ya Kati, ambao wanahatarisha maisha yao kwa kujaribu kuingia barani Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania. Watu wapatao 1,800 wameangamia katika safari za aina hiyo mwak huu pekee.
Mkutano huu wa kilele wa AU mjini Johannesburg umefanyika miezi mitano tu baada ya mwingine uliofanyika katika makao makuu ya umoja huo mjini Addis Ababa, Ethiopia Januari mwaka huu.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/ape
Mhariri: Sudi Mnette