AU kuimarisha juhudi za amani ya Libya
10 Februari 2020Katika mkutano huo wa siku mbili chini ya kauli mbiu ''Kukomesha vita barani Afrika'' viongozi na wawakilishi kutoka kote Afrika wamezitaka pande zinazopigana nchini Libya kufikia makubaliano ya kuweka chini silaha.
Hata hivyo Umoja wa Afrika umelalamika kwa kuachwa nje katika kusaka suluhisho katika mzozo huo ambao umedumu kwa zaidi ya miaka saba sasa, AU inasema michakato yote ya UN, imeendelezwa hasa na mataifa ya Ulaya pekee. Lakini Chergui alieleza kuwa umoja huo utaunga mkono makubaliano ya kuweka chini silaha ya pande hasimu.
''Kwa wakati huu, ni Umoja wa Mataifa (UN) unaotuhitaji sisi (AU), mashirika haya lazima yashirikiane kwa lengo hilo "amani ya Libya" Amesema Smail Chergui, mkuu wa baraza la usalama la AU; wakati akizungumza na wanahabari leo Jumatatu mjini Addis Ababa, kwenye mkutano wa kilele wa AU wa awamu ya 33.
Libya imegubikwa na mapigano ya makundi kadhaa ya kujihami tangu jumuiya ya kujihami ya NATO kumuondoa madarakani rais wa kimla Moamer Gadhafi, mnamo mwaka 2011.
Wakati huo Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres amesema anafahamu masikitiko ya Umoja wa Afrika kwa kutohusishwa katika masuala ya mzozo wa Libya.
Cyril Ramaphosa, rais wa Afrika kusini ambaye anachukua hatamu ya uenyeiti wa umoja huo amesema atazingatia masuala ya kurejesha amani nchini Libya.
Nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika imekumbwa na mapigano kati ya mbabe wa kivita Khalifa Haftar anaedhibiti maeneo ya mashariki wa nchi hiyo na serikali ya Tripoli inayoungwa mkono na Umoja wa mataifa.
Majadiliano ya kusitisha mapigano kati ya pande hasimu yalikamilika jumamosi bila kufua dafu ya kusainiwa kwa makubaliano. Umoja wa mataifa umependekeza Februari 18 kama siku kufanyika tena kwa mazungmzo hayo.