1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Atletico na Real kuumana katika Super Cup Uhispania

18 Agosti 2014

Mabingwa wa ligi kuu ya Soka Uhispania Atletico Madrid wana nafasi ya kulipiza kichapo walichopewa na Real Madrid katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati watakapokutana katika Super Cup

https://p.dw.com/p/1CwVM
Real Madrid vs. Atletico Madrid Spanien Liga Primera Division
Picha: picture-alliance/dpa

Licha ya kuwa na msimu bora zaidi katika historia ya Atletico, vijana hao wa Diego Simeone bado wameumizwa kichwa kutokana na kuondoka kwa wachezaji kadhaa muhimu msimu huu baada ya Filipe Luis na Diego Costa kujiunga na Chelsea huku naye mlinda lango Thibaut Courtois akirejea uwanjani Stamford Bridge baada ya kucheza misimu mitatu kwa mkopo.

Pesa walizopata kutokana na mauzo ya nyota hao zimewanunua Mario Mandzukic kutoka Bayern, Raul Jimenez wa Mexico na Antoine Griezmann kutoka Real Sociedad.

Atletico Madrid Mario Mandzukic 24.07.2014
Picha: picture-alliance/dpa

Nao miamba Real Madrid hawajadorora hata baada ya kushinda taji lao la kumi la Ulaya. Walitumia fedha nyingi kuwaleta Santiago Bernabeu nyota wa Kombe la Dunia James Rodriguez, Toni Kross na mlinda lango Keylor Navas. Mchuano wa kesho utachezwa uwanja wa Bernebeu, huku wa marudiano ukiwa nyumbani kwa Atletico Vicente Calderon Ijumaa usiku

English Premier League

Ni siku mbili tu baada ya ligi kuu ya Soka Uingereza, English Premier League kufungua pazia zake, na tayari ukiangalia kileleni mwa msimamo wa ligi, hauwezi kushangazwa na majina yaliyoshika usukani wa mapema. Manchester City walianza kampeni ya kulitetea taji kwa ushindi wa magoli mawili kwa sifuri ugenini dhidi ya Newcastle. Liverpool waliomaliza kama makamu bingwa walianza maisha mapya bila ya nyota wao Luis Sueret, na kupata ushindi wa magoli mawili kwa moja dhidi ya Southampton nyumbani Anfield, licha ya kutokwa na jasho. Arsenal pia walipambana na kupata ushindi wa magoli mawili kwa moja dhidi ya Crystal Palace. Manchester United walianza msimu kwa kujikwaa, baada ya kuduwazwa katika uwanja wao wa nyumbani mikononi mwa Swansea waliowafunga magoli mawili kwa moja.

Hii ina maana kocha mpya Louis Van Gaal ana kibarua cha kufanya ili kuirejesha timu hiyo katika kiwango cha juu. Hii leo Chelsea itaanza kampeni yake kwa kumenyana ugenini na Burnley ambao wamerudi katika ligi kuu baada ya kuwa nje kwa miaka mitano.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu