1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wapatao 85 wauwawa mjini El-Fasher Sudan

22 Mei 2024

Shirika la madaktari wasio na mipaka linasema watu wasiopungua 85 walikufa katika hospitali ya mji wa El-Fasher, jimbo la magharibi la Sudan la Darfur, tangu mapigano yalipozuka upya kati ya pande zinazohasimiana Mei 10.

https://p.dw.com/p/4g8eU
Wodi ya hospitali ya El Fasher ikiwa imejaa majeruhi wa vita
Wodi ya hospitali ya El Fasher ikiwa imejaa majeruhi wa vitaPicha: ALI SHUKUR/AFP

Mkuu wa programu ya dharura yashirika la Madaktari wasio na mipakanchini Sudan, Claire Nicolet, amesema siku ya Jumatatu pekee waathiriwa tisa kati ya 60 waliopokelewa katika hospitali hiyo kwa jina Southern Hospital, kwa ajili ya matibabu, walikuwa wamekufa kutokana na majeraha waliyokuwa wameyapata. Claire ameongeza kusema katika kipindi cha tangu mapigano yalipozuka katika mji mkuu wa Dafur Kaskazini wa El-Fasher, hospitali hiyo imepokea wahanga 707 wa vita na 85 kati yao wamekufa.

Kwa zaidi ya mwaka mmoja, mapigano yameendelea kati ya jeshi la serikali likiongozwa na mkuu wa jeshi, Abdel Fattah al- Burhan, na wapiganaji wa kikosi cha Rapid Support Forces, kinachoongozwa na naibu wake wa zamani, Mohamed Hamdan Daglo.

El-Fasher ni mji mkuu pekee katika eno kubwa la kaskazini la Darfur ambalo haliko chini ya wapiganaji wa RSF na ni eneo muhimu la utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa eneo ambalo linakaribia kutumbukia katika baa la njaa.

Soma pia: Watoto 13 wafa kila siku kwa utapiamlo Darfur - MSF

Mwezi huu, eneo hilo limekuwa uwanja wa makabiliano makali, licha ya miito kutolewa mara kwa mara kutoka wa Umoja wa Mataifa kuwataka wapiganaji waunusuru mji huo.

Watu walioshuhudia yanayoendelea huko wameripoti mashambulizi ya mara kwa mara ya makombora na milio ya risasi kutoka pande zote zinazopigana, pamoja na mashambulizi ya kutokea angani kutoka kwa jeshi la serikali.

Uharibifu unaoshuhudiwa El Fasher kutokana na vita
Uharibifu unaoshuhudiwa El Fasher kutokana na vitaPicha: AFP

Wakiwa wamenasa katika nyumba zao, wakazi wengi hawawezi na wanakosa ujasiri kuyakabili machafuko mabarabarani kuwapeleka wapendwa wao hospitali kupata matibabu.

Changamoto katika utoaji wa matibabu na huduma

Shirika la Madaktari wasio na Mipaka limesema wahanga wanaofanikiwa kufika hospitali ya Southern wanahudumiwa na daktari mmoja mtu mtaalamu wa upasuaji, hali inayoiweka hospitali hiyo katika shinikizo kubwa mno.

Kote nchini Sudan vita hivyo vimeharibu asilimia 70 ya vituo vya afya na kusababisha shinikizo kwa vituo vingine vilivyosalia.

Mkuu wa programu ya dharura ya shirika la Madaktari wasio na mipaka nchini Sudan, Claire Nicolet, amesema wana mahitaji yatakayotosha kuwahudumia wagonjwa kwa siku 10 tu katika hospitali ya Southern, huku akizihimiza pande zinazopigana zitoe njia za kupitia kuwawezesha kwenda kuchukua shehena nyingine za mahitaji.

Kikosi cha RSF kimesema kitafungua njia salama za kutokea mji wa El-Fasher huku kikiwataka wakazi wa mji huo waepuke maeneo ya mapigano na yale yanayoweza kulengwa katika mashambulizi ya kutokea angani, na wasitilie maanani miito ya kihasidi inayotolewa kuwashawishi wakazi na kuwatumbukiza katika moto wa vita.

Kwa mujibu wa wataalamu wa Umoja wa Mataifa, tangu vita vilipoanza, maelfu kwa maelfu ya watu wameuwawa, wakiwemo watu 15,000 katika mji mmoja wa Darfur Magharibi.

Kulingana na takwimu za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa, takriban watu milioni tisa wamelazimika kuyakimbia makazi yao. Kufikia mwisho wa mwezi Aprili, Darfur Kaskazini pekee iliwakaribisha watu wapya zaidi ya nusu milioni waliolazimika kuzikimbia nyumba zao mwaka uliopita.

(afp)