Assange azungumza hadharani kwa mara ya kwanza
1 Oktoba 2024Assange amesema aliachiwa huru baada ya miaka mingi kifungoni pale alipokiri makosa ya kuwa "mwandishi wa habari", katika hotuba yake amesisitiza na kuonya kwamba uhuru wa kujieleza sasa uko hatarini kutumbukia gizani.
Akizungumza mbele Baraza la haki la Ulaya, lenye makao yake makuu mjini Strasbourg, katika maoni yake ya kwanza ya umma tangu kuachiliwa kwake Assange amesema hayuko huru leo kwa sababu mfumo ulifanya kazi, lakini yuko huru leo baada ya kukaa kifungoni kwa miaka mingi kwa sababu alikiri kosa la kuwa mwaandishi wa habari.
Soma pia: Assange arejea nchini mwake baada ya kuachiliwa huru
Bunge la Baraza la Ulaya (PACE) lilikuwa limetoa ripoti ikielezea kusikitishwa na jinsi Assange alivyoshughulikiwa akiwa kifungoni, likisema kuwa ilikuwa na "athari za kutisha kwa haki za binadamu".
Alitumia muda mwingi wa miaka 14 iliyopita aidha akiwa amejifungia katika ubalozi wa Ecuador mjini London ili kuepuka kukamatwa, au kufungwa katika Gereza la Belmarsh.
Uhuru wa kujieleza
Na mwezi Juni aliachiliwa chini ya makubaliano ya rufaa, baada ya kutumikia kifungo kwa hatia ya kuchapisha mamia ya maelfu ya nyaraka za siri za serikali ya Marekani.
"Hatimaye nilichagua uhuru badala ya haki isiyotekelezeka baada ya kuzuiliwa kwa miaka na kukabiliwa na kifungo cha miaka 175."
"Haki kwangu sasa imezuiwa kwani serikali ya Marekani ilisisitiza kuandika katika makubaliano yake ya maombi kwamba siwezi kufungua kesi katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu au hata ombi la Sheria ya Uhuru wa Habari juu ya kile ilichonifanyia kutokana na ombi la uhamisho sababu nilikiri kosa la uandishi wa habari."
"Natumai ushuhuda wangu leo unaweza kutumika kuangazia udhaifu wa ulinzi uliopo na kuwasaidia wale ambao kesi zao hazionekani sana lakini ambao wako katika hatari sawa."
Nini hatma yake?
Hata hivyo kesi ya Assange inasalia na utata mkubwa. Wafuasi wanamsifu kama bingwa wa uhuru wa kujieleza na kusema aliteswa na mamlaka na kufungwa jela isivyo haki. Wapinzani wanamwona kama mwanablogu mzembe ambaye uchapishaji wake usiozingatia hati nyeti uliweka maisha ya watu katika hatari na kuhatarisha usalama wa Marekani.
Kwa sasa Assange bado anaendelea na juhudi za kupata msamaha wa rais wa Marekani kwa kuhukumiwa kwake chini ya Sheria ya Ujasusi.
Rais wa Marekani Joe Biden, ambaye huenda akatoa msamaha kabla ya kuondoka madarakani Januari mwaka ujao, amewahi kumtaja mwanablogu huyo kama "gaidi".