Assad awaambia waasi kamwe hawatamshinda
21 Septemba 2012Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zinasema zina wasiwasi kwamba Iran inavunja vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Syria, kwa kuupelekea utawala wa Assad shehena za silaha.
Mataifa hayo manne ya Magharibi yamesema katika matayarisho ya Mkutano wa 67 wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa, kwamba yataongeza mbinyo wao kwa utawala wa Assad na kuzitaka Urusi na China zisiwe tena kikwazo.
"Hatutaacha kuwakumbusha wanachama wengine kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba lazima waondoe kinga yao waliyouwekea utawala wa Assad. Lakini lazima tuelewe kwamba hadi sasa, Urusi na China hazijaonesha nia hiyo, jambo ambalo linatusikitisha na tunalikosoa vikali." Amesema Guido Westerwelle, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani.
Assad asema waasi hawawezi kushinda
Ndani ya Syria kwenyewe hakuna dalili yoyote inayoonesha kuwa mapigano yatamalizika karibuni. Rais Assad amewaonya wapinzani wake kwamba hawatafanikiwa kumuondoa madarakani, huku pia akiwalaumu majirani wa Syria kwa kuwapa silaha waasi.
Katika mahojiano na gazeti la Al Ahram Al Arabi la Misri, Assad ameurejea msimamo wake kuwa kinachofanywa na waasi hao ni ugaidi, na amezilaumu wazi wazi Qatar na Saudi Arabia kwa kuwatumia waasi ili kurejelea kile kilichofanyika Libya. Kuhusu Uturuki, Assad amesema nchi hiyo imepoteza mengi kwa kushirikiana na upinzani dhidi yake.
Mahojiano hayo yatakayochapishwa kikamilifu kwenye toleo la kesho (22.09.2012) ni ya kwanza kufanywa na Assad na gazeti la Misri ndani ya kipindi cha miaka mitatu.
Katika siku za karibuni, Misri imejitokeza kuwa mpinzani wa wazi wa utawala wa Assad, ambapo Rais Mohammed Mursi ametoa wito wa kusaidiwa kwa upinzani dhidi ya Assad.
Waasi waelekeza mashambulizi kwa ndege za jeshi
Katika medani ya vita, taarifa zinasema kwamba helikopta za kijeshi zimepambana na waasi karibu na kambi za kijeshi alfajiri ya leo huko Aleppo. Shrika la Haki za Binaadamu la Syria, lenye makao yake nchini Uingerez, limesema mapigano hayo yametokea karibu sana na uwanja wa ndege wa kijeshi kwenye kambi ya Hanano.
Wilaya nyengine kadhaa katika mji huo mkubwa kabisa wa kibishara, zikiwemo za Sakhur na Bustan al-Qasr, zilishambuliwa usiku mzima, huku mapigano mengine yakiripotiwa karibu na uwanja wa ndege wa jeshi wa Meng.
Viwanja vya ndege vya jeshi vimekuwa shabaha kuu ya waasi katika siku za hivi karibuni, katika wakati ambapo jeshi limeongeza matumizi ya ndege na helikopta kuwashambulia.
Miripuko pia imesikikana kutoka upande wa kaskazini magharibi mwa mji mkuu, Damascus, huku jimbo la kati la Homs, mji wa mashariki wa Deir Ezzor na jimbo la kusini la Daraa yakishuhudia mashambulizi makali ya mabomu na mizinga.
Kiasi cha watu 225 waliuawa jana peke yake, ambapo 140 kati yao ni raia, 39 waasi, na wanajeshi 46 wa serikali.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Othman Miraji