Askofu, Imam CAR washinda tuzo ya amani
2 Septemba 2015Askofu mkuu Dieudonne Nzapalainga na kiongozi wa kiroho wa Kiislamu Imam Kobine Lyama (pichani juu) kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati, na wanafunzi wanaharakati Rakotonirina Mandimbihery Anjaralova, Lumbela Azarias Zacarias na Balorbey Theophilius Okulu, ndiyo washindi wa tuzo hiyo ya heshima iliyotolewa katika mji wa kusini-magharibi mwa Ujerumani wa Aachen jana Jumanne.
Nzapalainga na Layama wametambuliwa kutokana na ushiriki wao katika mchakato wa amani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Viongozi hao wawili wamekuwa wakizihamasisha jamii zao kutafuta suluhu ya amani kwa mgogoro unaoendelea katika nchi yao, moja ya maskini zaidi duniani. Askofu mkuu Dieudonne amesema tuzo hiyo ni heshima kwa watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaoamini katika amani, maridhiano, na kuishi pamoja kwa mani.
"Siku ya leo ni ya kipekee kwa watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambao wamefanya juhudi za kurejesha amani, na leo juhudi zao zimetambuliwa. Tunaitoa wakfu tuzo hii kwa wote waliopoteza maisha yao bila hatia. Tunaamini damu yao itakuwa mbegu zitakazoiotesha upya Jamhuri ya Afrika ya Kati, alisema Askofu Dieudonne.
Tashihisi ya matumaini
Imam Kobine alisema tuzo hiyo itaongeza hamasa na kuwaonyesha raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na ulimwengu kwa ujumla, kwamba hata katika mazingira ya vita inawezekana kujifunga kwa amani. Moja wa waandaji wa tuzo hiyo Leila Vannahmes, amewataja viongozi hao wawili kuwa ni tashihisi ya matuimani.
Wanafunzi watatu wa kujitolea kutoka Madagascar, Msumbiji na Ghana wametambuliwa kwa juhudi zao za kuwasaidia wakimbizi waliokwama katika mji wa Oujda nchini Morocco. Wanafunzi hao walikuwa wanafadhiliwa na Kanisa la Kinjilisti na walikuwa wakiwasaidia wahamiaji wasio na makaazi kwa kuwapatia maji, chakula na dawa.
Balorbey Theopilius Okulu, moja wa wanafunzi hao anaetokea nchini Ghana alisema wanachokifanya hasa ni kuwapatia msaada wa kiutu watu wanaotoka mataifa mbalimbali, ambao wamechoka, waliopatwa na kihoro na kuathirika kisaikolojia.
"Wanataka kutimiza ndoto ya maisha bora wakitokea katika mazingira tofauti, baadhi wakikimbia vita, migogoro, ugumu wa maisha na baadhi ugaidi katika mataifa yao, alifafanua mwanafunzi huyo ambaye kundi lake linafadhaliwa na kanisa la Kiinjilisti.
Akizungumza katika hotuba yake ya kusifu wakati wa hafla ya kukabidhi tuzo hiyo mjini Aachen, mwana thiolojia na askofu wa zamani Margot Kässmann, alisema washindi hao ni mifano inayong'ara ya tabia ya kiutu katika uliwemgu ambao unazidi kukosa utu, huku akiutuhumu Umoja wa Ulaya kwa kufumbia macho ukiukaji wa haki za binaadamu kwenye mipaka yake.
Ulaya inapoteza dira yake
Akiyakosoa mataifa ya Umoja wa Ulaya yanayowafukuza wakimbizi, Kässmann alionya kuwa Ulaya ilukuwa inatupa mafanikio yake, ambayo kwayo Umoja wa Ulaya ulipatiwa tuzo ya amani ya Nobel. Mkutano wa maaskofu wa Ujerumani ulisema tuzo ya Aachen ni ushahidi tosha juu ya mchango wa amani miongoni mwa dini mbalimbali.
Shirika la ustawi wa kijamii la kikatoliki "Missio", ambalo linawafadhili viongozi wa kidini Nzapalainga na Layama katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, lilisema tuzo hiyo inahimiza utekelezaji wa miradi inayowasiaidia kulinda hadhi ya wahamiaji.
Tuzo ya Amani ya Aachen inatolewa kwa watu wanaofanya kazi kusaka amani na kufanikiwa kujenga uelewa baina ya tamaduni tofauti. Tuzo hiyo ambayo inaambatana na zawadi ya kiishara ya fedha taslimu euro 1,000, inatolewa kila Septemba 1 kila mwaka tangu mwaka 1988.
Mwandishi: Sandrina Blanchard
Tafsiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Grace Patricia Kabogo