1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ARUSHA : Wakili wa Rwanda mbaroni kwa mauaji ya kimbari

2 Septemba 2006
https://p.dw.com/p/CDFq

Serikali ya Tanzania imesema leo hii imemkamata mwanasheria wa Rwanda anayetuhumiwa na serikali ya Rwanda kwa mauaji ya kimbari nchini humo hapo mwaka 1994.

Polisi imesema imemkamata Callixte Gakwaya ambaye ni wakili wa utetezi katika Mahkama ya Kimataifa kwa Uhalifu wa Rwanda ilioko Arusha kufuatia kutolewa kwa hati ya kukamatwa na serikali ya Rwanda hapo mwezi wa Februari.

Kamanda wa polisi wa mkoa Basilio Matei ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wakili huyo amekamatwa hapo jana na hivi sasa yuko kizuizini.

Kwa mujibu wa hati ya kukamatwa kwake Gakwaya ambaye anaongoza timu ya mawakili wa utetezi kwa watuhumiwa wa mauaji ya kimbari ambapo kesi yao itasikilizwa hapo mwezi wa Januari alisimamia vizuizi vya barabarani na kuuwa Watutsi wakati walipokuwa wakijaribu kuukimbia mji mkuu wa Kigali.

Pia anatuhumiwa yeye mwenyewe binafsi kuwauwa Watutsi waliokuwa wameomba hifadhi nyumbani kwake.