1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ARUSHA : Waasi wa Dafur wakutana

5 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBc6

Makundi ya waasi wa Dafur yaliogawika yamekuwa na mazungumzo mjini Arusha Tanzania ili kuwa na msimamo wa pamoja katika mazungumzo ya amani na serikali ya Sudan.

Mazungumzo hayo yamekuja siku nne baada ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kukubali kupeleka kikosi cha wanajeshi wa kulinda amani katika jimbo la vurugu la Dafur. Mazungumzo hayo yalioanza jana yanasimamiwa na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika na yanatazamiwa kuendelea hadi leo Jumapili.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson amesema baada ya waasi hao kufikia msimamo wa pamoja mazungumzo ya serikali ya Sudan yanaweza kuanza katika kipindi kisichozidi wiki nne.

Hata hivyo kundi la waasi la kiongozi mwenye ushawishi Abdel Wahid al Nur limesusia mazugumzo hayo kwa kudai kwanza yatimizwe masharti yao ikiwa ni pamoja na suala la malipo ya fidia, kuhakikisha watu wanarudi kwenye maeneo yao na usalama kwenye makambi ya wakimbizi.

Al Nur amesema kila siku kuna mauaji, kuna vifo, mamia ya watu wanakufa na kuuliwa na serikali ya Sudan kwa kushirikiana na wanamgambo wa Janjaweed huko Dafur na kwamba wanataka jumuiya ya kimataifa ikomeshe mauaji hayo.

Kufanikiwa kwa mazungumzo hayo kuko mashakani kutokana na kutoshiriki kwa viongozi wawili wa waasi akiwemo al Nur mwenyewe.

Mzozo wa miaka minne wa Dafur umegharimu maisha ya watu 200,000 na kuwapotezea makaazi wengine milioni 2.